DC Kibiti: Tunaendelea kupokea misaada kwa waathirika mafuriko

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:05 PM Apr 22 2024
Misaada ya kibinadamu kwa waathirika mafuriko Kibiti.
PICHA: JULIETH MKIRERI
Misaada ya kibinadamu kwa waathirika mafuriko Kibiti.

JUMLA ya watu 36,900; ambao ni waathirika wa mafuriko wilayani Kibiti, Mkoa wa Pwani; wanahitaji misaada wa kibinadamu, huku Serikali ikiendelea na awamu ya pili ya utoaji wa misaada hiyo.

Akizungumza na Nipashe Digital kwa simu, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Joseph Kolombo, amesema waathirika ni wale waoko makambini ambao ni watu 2,472; pamoja na 34,428 ambao wamepata hifahdhi kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki.

Kwa mujibu wa Kanali Macha, awamu ya pili ya utoa wa misaada hiyo kwa upande wa Serikali inaanza leo Aprili 22, 2024, na kwamba awamu ya kwanza iliwahusu watu makambini, ambako kulitolewa chakula cha siku saba, kwa wakazi hao wa kata tano zilizoathrika.

Aidha, amesema kuwa ofisi yake inaendelea kupokea misaada na kuifikisha kwa waathirika ambao wako katika kambi nne ambzo ni ile ya Kitumbini, Mtombori, Kibongoya na Mkwajuni. 

"Niendelee kuishukuru Serikali na wadau wanaoendelea kutuletea misaada ambayo hadi sasa tumepokea unga tani 76, maharage tani 17, na magodoro 742. Niizidi kuwaomba wadau  kujitokeza na kuwaahidi misaada yote waliyotoa itapelekwa kwa walengwa kama tunavyofanya," amesema.

Imeelezwa kuwa kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) ya jijini Dar es Salaam, ni moja ya wadau waliojitokeza kusaidia waathirika wa mafuriko katika Wilaya ya Kibiti.

Misaada iliiyotolewa ni wa mifuko 122 ya unga wa ngano ambapo mwakilishi wa SSB, Twaha Mkumba, amesema mkurugenzi wa kampuni hiyo ameguswa, akaona ni vema kuungana na Mbunge wa Jimbo la Kibiti, katika kusaidia waliokumbwa na mafuriko hayo.

Akizunguza kwa niaba ya mbunge wa jimbo hilo, Diwani wa Viti Maalum, Zainab Chitanda ameishukuru kambuni hiyo, kwa kuwashika mkono wana-Kibiti waliofikwa na madhira ya mafuriko, sambamba kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazofanya  kuwasaidia waathirika hao.

Aprili 15, mwaka huu; Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alipokea misaada ya yenye jumla ya tani 300; zikiwa ni unga, mchele na maharage kutoka kwa Rais Samia.

Imeelezwa kuwa sababu kubwa ya mafuriko kwenye wilaya za Kibiti na Rufiji ambayo yalitokea Aprili 10, 2024, ni kuongezeka mtiririko wa maji katika Mto Rufiji, kulikosababishwa na mvua kubwa za El-Nino zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya nyanda za juu kusini.