DC Shaka aagiza polisi kuwakamata waliouza mlima kwa milioni 20

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 11:33 PM May 06 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka akizungumza na wananchi.

WATU wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msowero A, Petro Sanga (Paroko) na Awadh Ngajime kwa tuhuma za kuuza eneo la mlima, mali ya kijiji cha Msowero Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kwa sh. milioni 20.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, aliagiza kukamatwa kwa watuhumiwa hao mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa hadhara ambapo alikuwa akisikiliza kero za wananchi wa kata ya Msoweto A.

Alisema watu wengine 48 ambao wanaosadikiwa kuwa sehemu ya mtandao uliohusika kuuza kinyume na utaratibu jumla ya ekari 1158 za Kijiji zilizopo katika mlima huo wanaendelea kutafutwa.

Shaka alisema kumekuwa na wimbi la uvamizi wa maeneo ya ardhi unaoonekana kukithiri siku hadi siku na baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakihusika kuyauza kinyume na sheria.

"Tuna kata saba ndani ya wilaya hii zinaongoza kwa migogoro ya ardhi ikiwemo hii ya Msowero, mnaongoza mnavamia maeneo ya serikali, viongozi wapo mnashirikiana nao wengine kisha mnageuka mnasingizia viongozi wa wilaya mkoa na taifa kuwa wanakuja kupora ardhi yenu kumbe ni uongo," alisema na kuongeza kuwa;

"Mmeuza mlima kinyume na utaratibu ekari 1,158 zote mmevamia na kuuza hii ni mali ya serikali ya kijiji kisha mnageuka kushutumu wengine kumbe ninyi  wenyewe ndio wahusika, OCD huyomwenyekiti aliyeshiriki kuratibu mauziano na kulipwa Sh. 500,000 na huyu aliuza eneo la mlima kwa Sh 20,000,000 naondoka nao, pia naagiza watu wengine 48 waliohusika kwenye kuuza wajisalimishe polisi,  vinginevyo watafutwe popote walipo na wafikishwa kwenye vyombo vya sheria,".