KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amewataka Watanzania na serikali kuendelea kuenzi na kuwakumbuka mashujaa waliokufa wakati wa Vita ya Majimaji.
Nchimbi ameyasema hayo leo Songea alipotembelea Makumbusho ya Majimaji na kisha baadaye makaburi ya mashujaa 67 ambao kati yao 66 waliuliwa na wajerumani kwa kunyongwa na mmoja kwa risasi. Vita hiyo ilipiganwa kuanzia mwaka 1905-1907.
"Mashujaa waliozikwa hapa walikataa kutawaliwa waliona bora kufa kuliko kutawaliwa na wageni kutoka nje ya nchi. Tutaendelea kuenzi na kuthamini utamaduni wa Mtanzania" amesema Nchimbi Katika viunga vya makaburi hayo.
Akiwa Katika mkutano wa hadhara na wafuasi wa chama hicho baadaye baada ya kutembelea makumbusho hayo aliwataka Mabolozi wa chama hicho kuwekeza nguvu katika kuimarisha chama.
"Unapokwisha uchaguzi nongwa za uchaguzi hatuzitaki, unakuta uchaguzi imeisha miaka minne imepita we bado unanongwa mpaka leo aliyeshindwa ananongwa na aliyeshindwa ananongwa hii sio sawa itakigawa chama.
"Sio lazima kila mtu akuunge mkono wewe nani, ukiisha uchaguzi ungana na wote uliogombea nao shirikianeni mjenge chama" amesisitiza Dk. Nchimbi
Vilevile Balozi huyo, aliwataka wafuasi wa chama hicho kuchagua viongozi wanaotokana na CCM akisisitiza hakuna viongozi wa kulipeleka nchi mbali nje na chama hicho.
Awali katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM Amos Makalla alisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia ilani ya utekelezaji ya chama, uhai wa chama, maandalizi ya uchaguzi, na utatuzi wa kero za wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED