Dk Nchimbi kuanza ziara Njombe kesho

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 06:50 PM Apr 17 2024
Katibu wa Siasa na uenezi wa CCM mkoani Njombe, Josaya Luoga.
PICHA: ELIZABETH JOHN
Katibu wa Siasa na uenezi wa CCM mkoani Njombe, Josaya Luoga.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, anatarajia kuanza ziara ya siku mbili mkoani humo, ambapo atafanya mikutano ya hadhara mikubwa miwili Aprili 18 na 19.

Hayo yamesemwa leo na Katibu wa Siasa na uenezi wa chama hicho mkoani hapa, Josaya Luoga wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Dk Nchimbi atapokelewa katika viwanja vya stendi ya zamani vilivyopo Halmashauri ya Mji Makambako.

Pia imeelezwa kuwa katibu mkuu huyo atakutana na kuzungumza na viongozi wote wa chama hicho ngazi ya vijiji mpaka mkoa eneo la Hagafilo lililoo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe.

Amesema mkutano huo utakuwa maalum kwa sababu Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka atawasilisha utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitatu.

Amesema katika mkutano utakaofanyika mjini Makambako wananchi na wanachama wa chama hicho wafike kwa wingi ili kumsikiliza kwani atapokea changamoto mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi wake.

"Niwakaribishe wanachama na wananchi wote wa majimbo ya Makambako, Lupembe na Wanging'ombe ni majimbo jirani yanapakana na Makambako ambapo mkutano huo utafanyika" amesema Luoga.