Doyo ajitosa kumrithi Hamad Rashid ADC

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:05 PM Jun 19 2024
Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo akirejesha fomu kuwania Uenyekiti chama hicho.
Picha: Elizabeth Zaya
Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo akirejesha fomu kuwania Uenyekiti chama hicho.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Alliance For Democract Change (ADC), Doyo Hassan Doyo amejitosa kutia nia ya kugombea Uenyekiti wa Chama hicho kumrithi Hamad Rashid Mohamed ambaye amemaliza muda wake.

Ikumbwe kwamba Hamad Radhid pamoja na Doyo ni miongoni mwa waliokihama Chama Cha Wananchi(CUF), na kuanzisha chama cha ADC baada ya kuibuka kwa mgogoro.

Kabla ya kushika nafasi hiyo ya Uenyekiti, Hamad Rashid alikuwa anakilea na mwanzoni mwa mwaka 2016 baada ya kufanyika uchaguzi alichaguliwa rasmi kukiongoza katika nafasi hiyo huku Doyo akichaguliwa kuwa Katibu Mkuu na mpaka sasa wawili hao wametumikia katika nafasi zao hizo kwa miaka 10.

Tayari Hamad Rashid alishatangaza kung'atuka katika nafsi hiyo ili kupisha kuchaguliwa mrithi wake kama Katiba ya chama hicho inavyotaka katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Alliance For Democract Change (ADC), Doyo Hassan Doyo .
Jana Doyo alirejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo mbele ya Kamati  ya uchaguzi ya chama hicho.

Mbali na Doyo, mwingine aliyerejesha fomu hiyo jana ni mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, Scola Kahana ambaye aligombea Ubunge jimbo la Kibaha Mjini mwa 2020 kupitia ADC.

Akipokea fomu hizo,  Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ADC, Innocent Siriwa aliwataka wagombea wote kufuata taratibu na kanuni za uchaguzi ili kulinda amani.

"Hatua hii inaonyesha ukomavu wa kisiasa hasa pale ambapo viongozi wanapokubali kuachia madaraka kwa mujibu wa kanuni na sheria za katiba bila kulazimishwa.
1

"Natoa wito kwa wagombea kuzingatia taratibu zote zilizopo ili itakapofika tarehe 29, mwaka huu twende kwenye uchaguzi ambao tuna imani utakuwa huru na haki," alisema Siriwa.

Akizungumza wakati akirejesha fomu hiyo, Doyo alisema ameona  anatosha  kugombea nafasi hiyo  na endapo atafanikiwa atapambana Ili kuendelea  kukiimarisha chama hicho kufikia viwango vya juu kwa kuzingatia kulinda amani na utulivu wa nchi. 

"Kutokana na uzoefu wa miaka 10 nilioupata kutoka kwa Mwenyekiti aliiyemaliza muda wake naahiidi kuyaendeleza mazuri yote hususan kuilinda katiba ya chama chetu.

Doyo alisema kuwa  endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo atakisaidia chama kusukuma ajenda za upatikanaji wa ajira,elimu Bora,na kupata wabunge wawakilishi watakaowakilisha wananchi katika changamoto zao bungeni.