Gwajima ataka wazazi kufanya vikao kubaini ukatili

By Paul Mabeja ,, Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:30 AM May 16 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.
Picha: Maktaba
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amewataka wazazi na walezi kuwa na utaratibu wa kufanya vikao vya familia ambavyo vitawasaidia kuzungumza na watoto wao ili kubaini vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa na jamaa wa karibu.

Aidha, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimeishauri serikali kutunga sera ya familia ili kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, udhalilisha watu na vifo vitokanavyo na matukio hayo.

Dk. Gwajima amesema anatamani kutembelea kila nyumba nchini ili kuona mihutasari ya vikao vya familia vinavyofanywa.

Amebainisha hayo jijini hapa kwenye maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani na uzinduzi wa Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto awamu ya pili (MTAKUWWA II).

Amesema moja kati ya sababu zinaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa ukatili wa kijinsia kwa watoto ni wazazi na walezi kutokuwa na muda wa kuzungumza na familia zao na kuweka muda mwingi kwenye utafutaji wa maisha.

“Familia zipaswa kufanya vikao wewe baba ndiye rais wa familia na mke wako ndiye waziri mkuu na watoto wenu ndiyo wabunge hivyo mnapaswa kuweka utaratibu wa kufanya vikao vya familia kuzunguza, ili kubaini mambo yanayo wakabili watoto na kuyafanyia kazi natamani hata ningekuwa na uwezo wa kutembelea kila familia ili niweze kudai mikhutasari ya vikao vya familia,” amesema.

Amesema tofauti za wazazi hazipaswi kuathiri malezi na makuzi ya watoto na kukimbilia mitaani.

Kadhalika, amesema jukumu la malezi ya familia ni wazazi, wanapaswa kuwajibika kwa kila kitu ili kuwasaidia katika mstari na kuwakinga na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema wizara yake itatoa ushirikiano wa kutosha kutekeleza Mpango kazi huo.

Vile vile, Mchengerwa amewataka wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuweka mikakati ya kudhibiti vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopistha Mallya, amesema vitendo vingi vya ukatili kwa watoto vinafanywa na watu wa karibu na kwamba wazazi wanapaswa kuacha tabia ya kulaza chumba kimoja watoto wao na wageni.

TAMWA YATAKA SHERIA

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya familia duniani yalioandaliwa na chama hicho kwa kushirikiana na Shirika la kuwezesha Jamii yani Society Empowerment Organ (SEO), Mkurugenzi wa TAMWA, Dk. Rose Reuben amesema sera hiyo itasaidia kuhuisha familia zinazodhorota kutokana na matukio hayo.

Amesema ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwapo ongezeko la ukatili wa jinsia kwa wanawake na wanaume, ukatili kwa watoto na ongezeko la nyumba zinazoendeshwa na mzazi mmoja kwa sababu moja ama nyingine.

“Ukatili wa watoto wa kike na wa kiume umeongezeka na unaripotiwa kila kukicha mpaka wengi wanajiuliza tutakuwa na taifa la namna gani hapo baadaye, maana watoto wengi wamebagazwa na ukatili, watakapokuwa watakuwa watu wa aina gani,” amesema Dk. Rose.

Amesema uchambuzi walioufanya kwenye sheria na kanuni zinazolenga kuzuia ama kukomesha ukatili wa jinsia, malezi na makuzi ya watoto wamegundua kuwa kuna ombwe la sera thabiti ya kuziunganisha familia kwa kuwajibisha wanafamilia katika malezi na kudumisha ulinzi.

Mkurugenzi wa SEO, Upendo Mwichande, amesema sera hiyo ni muhimu kwa kuwa itaweka uzito wa umuhimu wa taasisi ya familia kwa wanajamii na kwa serikali kuoongeza vipaumbele vyake katika mipango na matumizi katika taasisi hii.

Pia, itasaidia kuibua mijadala katika ngazi zote za kijamii kuhusu uandaaji, uwajibikaji na uwajibishaji wa walezi na wazazi katika familia. Hii itasaidia kuwaandaa wazazi na walezi wanaojiandaa kuanzisha familia.

Siku ya Familia inaandhimishwa kwa miaka 30 na mwaka huu Umoja wa Mataifa umeipa kauli mbiu ya 'Familia na Mabadiliko ya Tabia Nchi' huku hapa nchini imepewa kauli mbiu isemayo ‘Tukubali tofauti zetu kwenye Familia, Kuimarisha Malezi ya Watoto.’