Huduma za Visa zanasa kusuasua kwa intaneti

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:11 AM May 16 2024
Huduma za Visa kupatikana kwenye intaneti.
Picha: Maktaba
Huduma za Visa kupatikana kwenye intaneti.

WATUMIAJI wa miamala ya kibenki pamoja na ving’amuzi kwa siku ya tatu mfululizo wamepata tatizo la intaneti huku Ubalozi wa Marekani nchini ukisitisha huduma kwa umma.

Kurasa za kijamii pamoja na ujumbe wa simu, zimeendelea kutoa taarifa kwa wateja wake wanaotumia huduma hizo, wakati Ubalozi wa Marekani nchini ukitangaza kutoa huduma ya dharura kwa raia wake pekee.

“Kutokana na changamoto za kimtandao nchini, Ubalozi wa Marekani itafunga huduma kwa umma. Miadi yote ya konseli kuanzia Mei 14 na 15, itafutwa na kupangwa baadaye. Kitengo cha konseli kitafunguliwa kama kawaida, kwa ajili ya kuchukua VISA na huduma za dharura kwa raia wa Kimarekani,” umeeleza ukurasa wa Ubalozi huo katika mtandao wa Instagram.

Mmoja wa wateja, wanaotumia huduma za kibenki, ameimbia Nipashe kwamba, amepokea ujumbe unaosomeka: “Ndugu mteja kuna changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya huduma zetu kutokana na hitilafu ya mtandao wetu, wanaendelea kushughulikia tatizo hili. Asante,” ujumbe huo ulitumwa kwa mteja aliyejitambulisha kwa jina moja la Innocent.

Kadhalika, mtumiaji wa huduma ya king’amuzi, Baraka Haule, amesema ameshindwa kulipia kifurushi cha mwezi ambacho hujiunga kila baada ya siku 30.

“Nilipojitahidi kulipia huduma ya kifurushi, niletewa ujumbe mfupi wa maandishi kuwa huduma inakataa kulipia fedha katika mfumo, niwe mtulivu,” amesema Haule.

Aidha, wasambazaji wakuu wa huduma ya intaneti, kwenda kwa taasisi binafsi na umma, ikiwamo za kibenki wanakadiria hali kutengemaa baada ya siku sita kuanzia Jumapili lilipoanza tatizo, baada ya utulivu na usalama baharini.

Anna Bruno, mkazi wa jijini Dar es Salaam, amesema hitilafu hiyo imemwathiri kwa sababu huagiza bidhaa kutoka nje na kujitangaza na kufanya mauzo kupitia mitandao ya kijamii huku kwa siku akiingiza kiasi kisichopungua Sh. 80,000.

“Mfano mimi ni kawaida kila siku kuuza bidhaa kupitia mtandaoni, nina kundi maalumu la kuungana na wateja wangu nilichoshangaa jana ujumbe kutoka kwa wateja uliingia kwa kusuasua nikadhani sina kifurushi, niliingiza mauzo kidogo kama Sh. 20,000 tu,” ameeleza.

Jason Ambross, mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam, ameliambia gazeti hili kwamba kuna baadhi ya taarifa zinazotegemewa na wananchi kupatikana kwenye duka lake la ‘steshenari’, lakini tangu Jumapili hali ilikuwa tofauti.

“Ninatoa huduma za kutoa kopi, kuchapa, pia huwa naingia kwenye tovuti za umma kupata huduma, mfano taarifa ya ‘loss report’ siku hizi ni mtandaoni, wateja wangu hufika hapa, naifungua fomu kisha nawajazia taarifa, picha ikikamilika wananilipa Sh. 500 na hapo hapo serikali inaingiza Sh. 1,000 kupitia control namba, lakini tangu jana taarifa zinashuka taratibu sana au hazifunguki kabisa,” ameongeza.