Kampeni ya Holela-Holela Itakukosti yaungwa mkono na nchi zingine za Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:32 AM Jun 20 2024
Wataalamu wa afya kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, kati na kusini ambao wanaudhuria mkutano wa 14 wa Utendaji Bora pamoja na mkutano wa 30 wa Kamati ya Pamoja ya Ushauri ya Wakurugenzi (DJCC) wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wataalamu wa afya kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, kati na kusini ambao wanaudhuria mkutano wa 14 wa Utendaji Bora pamoja na mkutano wa 30 wa Kamati ya Pamoja ya Ushauri ya Wakurugenzi (DJCC) wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Wataalamu wa afya kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, kati na Kusini ambao wanaudhuria mkutano wa 14 wa Utendaji Bora pamoja na mkutano wa 30 wa Kamati ya Pamoja ya Ushauri ya Wakurugenzi (DJCC) wameunga mkono kampeini ya Holela-Holela Itakukosti ambayo inasisitiza mbinu kamilifu ya “Afya Moja" kushughulikia tatizo la Usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA) na magonjwa ya zuonotiki.

Kampeni ya "Holela-Holela Itakukosti," ambayo inamaana ya "uzembe unagharimu," inaonyesha uhusiano muhimu kati ya afya ya binadamu, afya ya wanyama, na mazingira. Kwa kutumia mkakati wa sekta mtambuka, kampeni hii inalenga kushughulikia sababu mbalimbali za kijamii zinazopelekea tatizo la UVIDA na magonjwa ya zuonotiki na ilizinduliwa mwishoni mwa mwezi Mei 2024, ikiwa ni ushirikiano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Makamu Rais (Mazingira), na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wa Breakthrough ACTION.

Kampeini ya Holela-Holela Itakukosti ilitambulishwa mwishoni mwa wiki kwa wataalam wa afya na viongozi mbali mbali kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika ambao wanakutana Jijini Arusha kwenye mkutano wa 14 wa Utendaji Bora pamoja na mkutano wa 30 wa Kamati ya Pamoja ya Ushauri ya Wakurugenzi (DJCC), ambapo kwa pamoja waliunga mkono na kupongeza kampeni hiyo na jitihada zake katika kupambana na UVIDA.

“Nchi nyingi za Afrka ambazo zinawashiriki kwenye mkutano huu wameonyesha nia ya kuiga mfano wa Tanzania katika kushughulikia changamoto za UVIDA kwa kutumia mtindo wa sanaa na kisayansi bila kuathiri maarifaa kwa watu wa kawaida”, alisema Mratibu wa Kitaifa wa UVIDA kutoka Wizara ya Afya, Emiliana Francis.

Katika Mkutano wa 14 wa Best Practices na Mkutano wa 30 wa Kamati ya Ushauri ya Pamoja ya Wakurugenzi (DJCC) uliofanyika Arusha, Shahada Kinyaga, Naibu Mkuu wa Mradi wa USAID Breakthrough Action Tanzania, alitoa uwasilishaji mfupi kuhusu kampeni mpya iliyoanzishwa hivi karibuni ya "Holela-Holela Itakukosti." Kampeni hii inalenga kuleta tabia chanya ili kukabiliana na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa yaani UVIDA na magonjwa yanayoweza kuenea kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (Magonjwa ya Zuonotiki) kwa kutumia mbinu ya Afya Moja.
Francis alisema kuwa baadhi ya nchi zimeonyesha kuguswa na KIDO – ambaye ni balozi wa kampeni ya Holela-Holela Itakukosti na kuomba kumpa mwaliko pamoja na bendi ya Wamwiduka (kundi la muziki wa kiasili liloshiriki kutengeneza wimbo wa holela holela itakukosti) ili kuwasaidia katika jitihada zao dhidi ya matumizi mabaya ya dawa kwenye nchi zao.

KIDO – ni mhusika ambaye anatambulika kwa vazi la rangi kama kidonge chekundu na njano kinachoashiria aina ya dawa za antibiotiki zinazotumiwa vibaya na wananchi.

Awali, Balozi Mpoki Ulusubisya ambaye ni Mkufunzi mtaalam wa masuala ya afya na udaktari alisema kuwa kukosekana kwa kanuni sahihi kuhusu uuzaji wa dawa za viua vijasumu, watu wengi wamekuwa wakitumia vibaya dawa na hivyo kujitibu kwa ugonjwa wowote wanaoupata bila ya kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya.

‘Tunaelekea katika njia ile ile kama ilivyokuwa kwa Chloroquine, dawa ambayo ilikuwa na ufanisi mkubwa katika kutibu malaria lakini haikusaidia kwa sababu ya matumizi mabaya’, alisema Balozi Ulusubisya.

Alisema kuwa watu wengi hutumia antibiotics kutibu magonjwa ya virusi bila ya kupata au kufuata maelekezo ya wataalamu, na wakati mwingine hutumia kipimo kidogo na matokeo yake bakteria hupata upinzani dhidi yao.
Baadhi ya Wataalamu wa afya kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, kati na kusini ambao wanaudhuria mkutano wa 14 wa Utendaji Bora pamoja na mkutano wa 30 wa Kamati ya Pamoja ya Ushauri ya Wakurugenzi (DJCC) wakifuatilia kwa umakini uwakilishaji wa kampeini ya kampeini ya Holela-Holela Itakukosti ambayo inasisitiza mbinu kamilifu ya “Afya Moja" kushughulikia tatizo la UVIDA na magonjwa ya zuonotiki. Wataalamu hao wafurahisha na kampeini hiyo na kuunga mkono huku wakisema wataiendeleza kwenye nchi zao walikotoka.