Kampeni ya madaktari bingwa wa Samia yafikia watu 20,900

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:45 AM May 22 2024
 Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Maktaba
Rais Samia Suluhu Hassan.

KAMPENI ya madaktari wa Rais Samia Suluhu Hassan iliyozinduliwa Mei 6, mwaka huu, mkoani Iringa, imetoa huduma katika halmashauri 56 ndani ya mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa kuwahudumia wagonjwa 20,922.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Englibert Kayombo, akizungumzia kampeni hiyo jana, alisema kati ya wagonjwa hao watoto ni 1,170, ambao walipata huduma mbalimbali. 

Kuhusu mafanikio ya kampeni hiyo, alisema mpango huo umeonyesha uhitaji mkubwa wa wagonjwa walioonwa na wataalam wa afya waliokuwapo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara. 

“Kwa sasa madaktari hawa wanatoa huduma katika hospitali za halmashauri. Lengo  halisi ni kufika maeneo ya chini kabisa ili kuwasaidia Watanzania wote. 

“Serikali inataka kupunguza kama si kuondoa kabisa changamoto za Watanzania, hivyo kupitia program mbalimbali za Wizara ya Afya, tunaamini kwa kiasi kikubwa itasaidia wananchi katika maeneo yote ambayo madaktari hawa watatoa huduma,” alisema Kayombo. 

Kayombo alisema mbali na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa, wataalam hao watatumia ujuzi wao kuwanoa wataalam wa afya katika maeneo watakayopita ili kuwasaidia katika utoaji huduma endelevu. 

Mikoa ambayo mpaka sasa madaktari bingwa wa Rais Samia wametoa huduma ni  Iringa, Njombe, Songea, Mbeya, Songwe, Lukwa, Manyara, Singida na Dodoma. 

Kampeni hiyo ilizinduliwa Mei 6, mwaka huu, mkoani Iringa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ambaye alisema wataalam hao wameangalia maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi kama vile madaktari bingwa wa afya ya uzazi na wanawake, watoto na watoto wachanga. 

Wengine ni daktari bingwa wa upasuaji, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na daktari bingwa wa usingizi na ganzi ambao kwa pamoja wanafikia 25 na watatoa huduma kwa siku tano za wiki.  

Kwa mujibu wa Kayombo, madaktari hao wiki hii wanatoa huduma Arusha, Kilimanjaro na Tanga, hivyo kuongeza idadi ya mikoa itakayokuwa imenufaika na huduma hiyo ya madaktari bingwa wa Rais Samia.

 Madaktari hao wamepiga kambi Muheza mkoani Tanga kwa siku nne na kuleta mafanikio makubwa ikiwamo kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma za kibingwa kwenye hospitali kubwa. 

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah, baada ya kuzindua kampeni hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Muheza iliyoko Kijiji cha Lusanga, alisema kambi hiyo imeonekana kuwa na tija kwa wananchi kwa kuwa imepunguza gharama za kufuata huduma za kibingwa nje ya wilaya. 

Timu hiyo ya madaktari bingwa waliowasili mkoani Tanga wameanza kutoa huduma katika hospitali za wilaya zote mkoani humo huku wito ukitolewa kwa wananchi kujitokeza kupata matibabu ili kupunguza ghalama kwa kufuata huduma hizo katika hospitali kubwa nchini.

 Nipashe  ilifika katika Hospitali ya Wilaya ya Muheza  na kushuhudia huduma zikiendelea kutolewa kwa wagonjwa wenye matatizo mbalimbali chini ya uangalizi wa madaktari hao bingwa.  

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Dk. Juma Mombokaleo, alisema wagonjwa  wameendelea kujitokeza katika hospitali hiyo kupata huduma mbalimbali wakiwamo  wanawake na wenye changamoto ya uzazi. 

Imeandikwa na Mwandishi Wetu (DAR) na Steven William (MUHEZA)