Kanuni kuwabana wazalishaji chupa za plastiki, vifungashio

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:40 AM Apr 19 2024
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo.
PICHA: MAKTABA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, amesema serikali imepanga kutunga kanuni mpya za utunzaji wa mazingira kwa wazalishaji wa vinywaji vinavyotumia chupa za plastiki na vifungashio.

Miongoni mwa kanuni ni pamoja na wazalishaji wa bidhaa hizo kukusanya chupa zilizotumika kutoka mitaani ili kutunza mazingira.

Jafo amesema hayo jijini hapa alipokuwa akifungua kikao cha majadiliano na wazalishaji wa bidhaa zinazofungashwa kwa plastiki kilichohusu kupata ufumbuzi wa tatizo la kuzagaa kwa chupa za plastiki mitaani.

Amesema madhara ya uharibifu wa mazingira kutokana na matumizi ya chupa za plastiki yanaathari nyingi kwa viumbe hai ikiwamo samaki baharini.

Pia amesema bidhaa za plastiki zina madhara kwa mifugo na katika sekta ya utalii zinachafua mazingira ya hifadhi.

“Kila kampuni ihakikishe kuwa chupa zake hazipo mtaani baada ya matumizi. Na uamuzi huu utaongeza fursa ya ajira kwa vijana na wanawake watakaojiajiri kwa kuokota chupa hizo,” amesema Jafo.

“Marufuku hiyo inakwenda kutekelezwa kwa kuunda kanuni ya kuhakikisha ukusanyaji wa chupa za plastiki zilizotumika sio tena jambo la hiari,” amesema Jafo.

Amemwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mazingira na taasisi zake kuhakikisha kanuni hizo zinakuwa tayari kabla ya kukamilika kwa vikao vya bunge la bajeti ambavyo vinaendelea jijini hapa.

Pia  amelitaka Baraza la Taifa la Hofadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais kusimamia vyema kanuni za mazingira zilizopo.

Amewataka wazalishaji hao kubuni vifungashio vinavyoweza kuharibiwa au kuzalishwa upya badala ya kuendelea na plastiki.

Amezipongeza kampuni zilizokamilisha taratibu za urejeshaji wa chupa za rangi na kuzitaka ambazo bado zianze kufanya hivyo.

Jafo amesema inaleta taswira mbaya kwa watalii wanaofika nchini na kutembelea fukwe mbalimbali kuona chupa za plastiki zikizagaa.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Mazingira, Christina Mndeme, amesema ofisi yake inaendelea kuratibu na kusimamia masuala ya uhifadhi wa mazingira kuhakikisha kuwa yanatunzwa na kuwa salama kwa afya na ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

“Katika kuhakikisha kuwa uchafuzi wa mazingira unadhibitiwa, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zikiwemo kuandaa sharia, kanuni na miongozo inayosimamia hifadhi ya mazingira,” amesema.

Amesema ofisi hiyo inaendelea kusimamia katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki la  Juni Mosi, 2019 na kuwa la mafanikio makubwa licha ya kuwapo changamoto ya taka za plastiki.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa NEMC, Dk. Thobias Richard, amesema licha ya katazo hilo kuna baadhi ya viwanda na wafanyabiashara wanafanya udanganyifu kwa kuzalisha bidhaa za plastiki zisizo na viwango.

“NEMC tulizunguka kwenye viwanda 89 vinavyozalisha chupa na mifuko ya plastiki, vipo 30 ambavyo tulikuta vina changamoto tukachukua hatia ikiwamo kuwapa elimu ili warudi kwenye utaratibu wa kisheria, tulienda kwenye fukwe, masoko 20 tukachukua hatua ka watu 89 walioshindwa kutekeleza agizo la serikali,” amesema.