Kauli ya Askofu Shoo rushwa ya aibu yaibua wadau uchaguzi

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 08:27 AM May 28 2024
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk. Fredirick Shoo
Picha: Nipashe Digital
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk. Fredirick Shoo

KAULI ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk. Fredirick Shoo juu ya "rushwa ya aibu katika uchaguzi" imeibua wadau wa siasa, wakitaka Watanzania wawe kitu kimoja kuchagua viongozi wenye maadili na si wanaotumia fedha chafu.

Juzi Askofu Dk. Shoo alitaja ubinafsi kuwa ni sumu mbaya iliyofikisha baadhi ya watu kwenye hatua ya kutaka fedha chafu ili kupata madaraka kwa lengo la kujinufaisha wao na familia zao badala ya maslahi ya taifa.

Katika mazungumzo na Nipashe kuhusu kauli hiyo jana; Mchambuzi wa Siasa, Abbas Mwalimu, alisema alichokisema Askofu Shoo si jambo geni, linahusiana na maadili, hasa wakati wa uchaguzi.

"Kinachotokea ni kwamba ukichagua kiongozi ambaye ametumia fedha zake, maana yake ni kwamba atakapopata uongozi atahitaji kurudisha fedha yake, sasa zinarudi vipi? Ndio Askofu Shoo, anakieleza.

"Hatuna kiongozi ambaye tunaweza kumwajibisha, tutakuwa na kiongozi ambaye anaweza kujiwajibikia mwenyewe, kwa sababu tayari ameshatulipa kwenye kura, ni kama ukienda dukani ukanunua bidhaa, mkate na ukishaununua unabaki kuwa wako, ameshawanunua watu kama bidhaa," alisema Abbas.

Alisema kuwa alichokisema Askofu Dk. Shoo kinaakisi na Katiba, Ibara ya 8(1)(a) inaelekeza "wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba".

Pia alirejea kifungu cha 1(b) na (c) vya ibara hiyo ya Katiba kinachoeleleza kuwa lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi na serikali itawajibika kwa wananchi.

"Abbas alisema, "anachosema Askofu Shoo ni kwamba tuchague viongozi ambao tunaweza kuwawajibisha. Wakati wa kampeni ulituambia utatekeleza a, b, c, atuambie ametekeleza nini ndani ya miaka miwili?

“Wabunge wanaweza kumwajibisha Rais, wana uwezo kumwajibisha waziri mkuu kwa mujibu wa Katiba, pia wana uwezo kumwajibisha makamu wa rais, spika, jiulize nani anamwajibisha mbunge mwenyewe? Ni mwananchi.

"Inatakiwa mwananchi amhoji mbunge wake, mbali na ilani ya chama cha siasa, kuna ilani ya mbunge, mwananchi amwulize mbunge wake, askofu anamaanisha kama kura zinanunuliwa kwa rushwa, ni vigumu kumwajibisha kiongozi aliyechaguliwa na ameingia katika uongozi kwa rushwa," alisema Abbas.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya, alisema anaunga mkono hoja ya Askofu Dk. Shoo, kwamba kiongozi anayepatikana kinyume cha maadili hafai kuongoza umma.

"Kiongozi wa aina hii akipata uongozi atahakikisha anatumia rasilimali za umma kurejesha fedha zake. Atakuwa mtu ambaye hana sifa ya uongozi, kwa sababu atakuwa amenunua uongozi.

"Uongozi bora ndio rasilimali namba moja ya maendeleo ya taifa lolote, maana yake mtu wa ovyo hana sifa za uongozi. Kiongozi bora ana ubunifu, mwajibikaji, akiona ametoa fedha yake yeye hana shida anawaza kutafuta fedha kubwa ili aje ahonge zaidi," alisema Dk. Ananilea.

Alisema kwamba wakati nchi inaingia katika mfumo wa vyama vingi, lengo lilikuwa kuboresha maisha, ingawa hadi sasa mfumo huo haujatimiza malengo hayo kutokana na baadhi ya viongozi kufanya anachokilalamikia Dk. Shoo.

"Wakati umefika sasa Watanzania tuamke. Kuna wanafunzi wanamaliza vyuo, hawana kazi, tuna rasilimali kibao. Askofu Shoo tunamwunga mkono kiongozi huyu wa kidini, mtu hata kama anawania uenyekiti, ubunge, udiwani, urais asipewe kama hana sifa," alihimiza Ananilea.

Mkazi wa Ukonga, jijini Dar es Salaam, Dk. Fredirick Shooakitoa maoni yake, alisema wananchi wanapenda kuwa na kiongozi ambaye anakuja kutatua changamoto zao ingawa baadhi ya matarajio hayo hayafanikiwi.

"Kiongozi ambaye mimi ninamhitaji ni yule ambaye ana jicho la kutukomboa, tena kwa masuala madogo tu mtaani. Kiongozi akiomba kura anashinda, akishapata uongozi hamwoni. Au unamchagua kiongozi huyu, analetwa mwingine, uchaguzi nao ni kama pata potea tu," alisema Daudi.

Juzi, Askofu Dk. Shoo alitoa wito kwa wanaoipenda nchi yao kuwa sauti moja kuhakikisha viongozi waliopo kwenye madaraka na mamlaka wawajibike kwa ajili ya ustawi wa taifa.

Alionya kuwa ndani ya vyama vya siasa kuna migongano mikubwa kiasi kwamba wengi hawajui mwelekeo ni wapi, shida kubwa akitaja ni ubinafsi; kila mtu anaangalia mambo yake na si ustawi wa kundi, nchi na vizazi vyake.

KUSOMA HOJA YA ASKOFU SHOO KUHUSU RUSHWA - Askofu Shoo aibuka na rushwa ya aibu