Kauli ya Makonda yapingwa vikali

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:18 AM May 28 2024
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya,(kulia) Profesa Askofu Victor Chisanga (katikati) na Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewajibu waliomwonya kutoa kauli wanazodai zinadhalilisha watumishi wa umma.

Amesema hatishwi na kauli zao na ni kama wanambembeleza na kumwongezea nguvu ya kufanya kazi.

Majibu hayo yamekosolewa vikali na baadhi ya viongozi na wadau wa siasa, wakimtaka ajitathmini kiutendaji.

Mei 24 mwaka huu, ilisambaa video fupi ikimwonesha Makonda akimhoji mtumishi mwanamke wilayani Longido, wakosoaji wakidai mkuu wa mkoa huyo alitumia lugha ya udhalilishaji dhidi ya mtumishi huyo.

Baada ya kusambaa kwa video hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT), walimwonya Makonda dhidi ya madai hayo ya udhalilishaji wanawake na watumishi wa umma.

Jana ikiwa ni muda mfupi baada ya Makonda kuwajibu wanaomkosoa, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya, alikosoa kauli ya Makonda, akisema kiongozi makini hadhalilishi wenzake bali anazingatia miiko, kanuni na taratibu za uongozi.

"Uongozi bora ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya taifa na kiongozi bora yeyote hatafuti umaarufu kwa kudhalilisha wengine, kiongozi bora anazingatia maadili, anaonya na kufuata misingi ya kazi. Hawezi kuongea maneno ya chumbani hadharani," alisema.

Dk. Ananilea alidai maneno ya Makonda kwa baadhi ya watumishi mkoani Arusha yanatweza utu wa wanaume na wanawake na hata yeye (Makonda), asingependa mke wake atolewe maneno makali mbele ya watu.

"Kiongozi bora siyo yule anayedhalilisha wenzake mbele ya wananchi kutafuta umaarufu, kiongozi bora anafuata misingi ya uongozi. Akumbuke kwamba yeye ni mwakilishi wa Rais, anapaswa kulinda haiba ya kiongozi aliyemteua," alisema.

Profesa Askofu Victor Chisanga (mstaafu wa Chuo Kikuu cha Ardhi) alidai utendaji wa Makonda unadhihirisha namna CCM imeshindwa kuhudumia wananchi.

Msomi huyo ambaye kwa sasa ni Askofu wa Kanisa la World United Alliance Church in Tanzania (WUAC-Tanzania), alisema: "Mungu aliniambia kwamba kazi ya Makonda ni nzuri na mbaya. Ni nzuri kwa sababu inaweka wazi kuharibika na kushindwa kazi kwa CCM na serikali yake na ni mbaya kwa sababu anaipa ‘oyee’ izidi kukaa madarakani wakati ni wazi haifai tena."

Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda, alipotafutwa na Nipashe jana, alikataa kuzungumzia kauli mpya ya Makonda dhidi ya "wanaopiga kelele" kwa madai kuwa hajaisikia.

"Sijui chochote, nilikuwa kwenye kazi zangu, subiri niangalie taarifa ya habari nione alichosema," alisema Mary.

Wiki iliyopita Mary alisema, "Nimesikitishwa sana na hawa viongozi mnaowateua, kunyanyasa na kudhalilisha watendaji wanawake kwenye sehemu zao za kazi. 

"Nimesikitishwa sana na kipande cha video kilichozunguka kule Longido, haikuwa jambo jema, si jambo zuri hata kidogo, kama wewe ni kiongozi mkubwa wa serikali unamwona mtendaji wako wa chini amekosea, huwezi kuwa na kauli na ulimi usio mzuri.

"Ni vizuri ukakaa nao ukazungumza nao, una nafasi ya kumwita na kumwambia kwa masuala ya udhalilishaji wanawake Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti hatutakubaliana nayo, haiwezekani, tunaomba tuheshimiwe wanawake, tena sisi ni watendaji wazuri kuliko hao wanaume."