Kaya 1,373 zahama kwa hiyari NCAA tangu 2022

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:51 AM May 28 2024
 Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhage Matinyi.
Picha: Mtandaoni
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhage Matinyi.

JUMLA ya kaya 1,373 zenye watu 8,364 zimekubali kuhama kwa hiyari katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) tangu mpango wa kuwahamisha kwa hiari ulipoanza Juni 2022.

Serikali imesema mpango wa kuwahamisha kwa hiyari kupitia elimu na uhamasishaji unaendelea ili kufikia idadi yote ya wakazi takribani 198,000 wanaotarajiwa kuhama kwenda katika vijiji vya Msomera wilayani Handeni, Saunyi wilaya ya Kilindi na Kitai, Simanjiro.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhage Matinyi, alisema uhamishaji huo unasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia NCAA.

 Alisema tangu mpango huo ulipoanza Juni, 2022, jumla ya kaya 1,373 zenye  watu 8,364 zimeshahama, kaya 1,248 zenye watu 7,547 zikienda Kijiji cha Msomera na kaya 125 zenye watu 817 katika vijiji vya Saunyi na Kitai.

 Alisema uhamaji huo pia ulihusisha jumla ya mifugo 36,457 ambapo 30,314 ilikwenda Msomera na 6,143 ikielekea kwenye maeneo mengine.

Ili kufanikisha mpango huo, serikali na NCAA ziliweka mkakati wa maalum wa uelimishaji, uhamasishaji na uandikishaji ukijumuisha timu ya viongozi na watendaji wa serikali za mitaa ndani ya NCAA.

 Alisema timu hiyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii imeshawafikia wananchi wengi wanaohusika na uhamaji hiari kupitia nyumba za ibada, minada, mikutano ya hadhara, viongozi wa kimila, watu maarufu na wenyeviti wa vitongoji na vijiji.

 Matinyi alisema mkakati huo unafuata maeneo yaliyogawanywa katika kanda tano za kaskazini, kusini, mashariki, magharibi na kati mwa Tarafa ya Ngorongoro ili kuhakikisha kata zote 11, vijiji vyake na vitongoji zinafikiwa.

 Alisema mpango wa serikali ni kujenga nyumba 5,000 kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambapo 2,500 zitajengwa katika Kijiji cha Msomera, Kitwai nyumba 1,500 na Saunyi nyumba 1,000.

Alisema katika Kijiji cha Msomera nyumba 1,000 zimeshakamilika, 737 zimeshakabidhiwa kwa wananchi na 263 zilizobakia ziko tayari kwa ajili ya kupokea kaya ambazo muda wowote kuanzia wiki ijayo zitapelekwa.

 “Nyumba nyingine 1,500 bado ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi ili kufikisha idadi ya nyumba iliyokusudiwa,” alisema Matinyi.

 Alisema pia nyumba nyingine 2,500 zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Kitwai na Sauni na upimaji wa viwanja umeshafanyika.

 Matinyi alisema hifadhi hiyo imeendelea kupokea idadi kubwa ya wageni ambapo kati ya Julai 2023 na Aprili 2024, ilifikia watalii 780,281.

 Alisema kupitia ugeni huo yamepatikana mapato ya Sh. bilioni 188.5 na kuvuka lengo la Sh. bilioni 155.4, akitamba ni matunda yaliyotokana na filamu ya The Royal Tour.