Kinana ashauri watendaji serikalini kutoa ahadi zinazotekelezeka

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:01 PM Apr 17 2024
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana, akizungumza na wananchi wa Mara.
Picha: Mauld Mbagga
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana, akizungumza na wananchi wa Mara.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahman Kinana ameshauri viongozi wa serikali kuacha kuahidi mambo ambayo hayajawekewa mipango, au wasiyojua kuwa utekelezaji wake utafanyika lini ili kuepusha malalamiko yanayotolewa na wananchi.

Kinana ametoa ushauri huo leo Wilayani Bunda, mkoani Mara, baada ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya maofisa wa serikali kuwataka wahame katika maeneo yao kupisha mradi wa maendeleo, wakidai kuwa hawajalipwa hadi sasa licha ya kwamba walishafanyiwa tathmini muda mrefu.

Wananchi hao wameonyesha kukerwa na kitendo cha maeneo yao kuchukuliwa na nyumba zao kubomolewa pamoja na kupewa masharti ya kutofanya shughuli zozote za kimaendeleo katika maeneo hayo ikiwemo Kijiji Cha Nyantwati.

Kutokana na malalamiko hayo Kinana amesema "Viongozi wa serikali kabla ya kuwahamisha wananchi ni vyema wakaeleza ni lini ahadi hiyo itatekelezwa, kama ni watu kuhama watahama lini, na fidia watapewa lini, hakuna sababu ya kutoa ahadi halafu inakaa miaka na miaka, kila kiongozi anakuja anaahidi anaondoka".