Kinana: Rais Samia amedhamiria kumtua mwanamke kuni kichwani

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:17 PM May 27 2024
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana akimkabizi mtungi wa gesi mmoja wa wananchi katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.
Picha: Maulid Mmbaga.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana akimkabizi mtungi wa gesi mmoja wa wananchi katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana amesema kampeni ya nishati safi iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kumtua mwanamke mzigo wa kuni kichwani na kumpa muda mwingi wa kujikita katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza mbele ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika  Kata ya Ngerengere, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, leo, Kinana amesema uamuzi huo wa Rais Samia unakusudia kusaidia kuwainua wanawake.

Aidha, Mbunge wa jimbo hilo Hamisi Taletale ametumia mkutano huo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na kushirikiana na kampuni ya Oryx kukabidhi mitungi ya gesi 800 kwa wananchi kwaajili ya kupikia.

"Uwepo wa nishati safi kwaajili ya kupikia ni matokeo ya sera na ubunifu wa Rais Samia, ambako mwaka jana alianzisha mchakato wa kuwatua akina Mama mzigo wa kuni, sambamba na kuanzisha mradi wa nishati safi na salama, amesema Kinana.

Ameongeza kuwa Rais Samia alitambua kwamba suala hilo linahitaji fedha nyingi, kuungwa mkono na dunia nzima na msaada wa watu wenye uwezo, na kwamba uongozi wake umedhihirisha yeye ni mtu wa vitendo, mbunifu na mwenye kutumia maarifa katika utendaji wake.

Aidha, ameeleza kuwa hivi karibuni Rais Samia alikuwa Ufaransa katika mkutano wa nishati safi ambao alikuwa Mwenyekiti Mwenza uliolenga kusaidia kumtua mama mzigo wa kuni, kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

“Kuna maelfu ya akina mama wanafariki dunia kwa sababu ya matumizi ya kuni na mkaa, karibu watu 50,000 wanafariki kila mwaka kwa sababu ya nishati isiyosalama. Rais Samia ameamua kuanza kampeni ya kuhakikisha kila nyumba inatumia gesi ya kupika.

“Nchi yetu ina umri wa miaka 60 jambo hili halijawahi kufikiriwa wala kubuniwa, lakini Rais Samia ameona umuhimu wake, inawezekana anawajali sana Watanzania lakini ni ukweli usiopingika anawajali sana akina mama, ndio maana amelichulikua jambo hili.

"Sote ni mashahidi Rais alianza na kampeni kubwa ya kumtua mama ndoo kichwani na ameanza miradi mikubwa ya maji nchi nzima na miradi hii inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Kuwatua akina mama ndoo na mzigo wa kuni, hii si kazi ndogo na haya ni mafanikio makubwa katika maisha ya Watanzania. Ninyi mnajua kina mama wakirahisishiwa kazi hii nchi itapiga hatua kubwa na nguzo ya familia ni mama,” amesema Kinana.

Akikabidhi mitungi hiyo Meneja Masoko wa Oryx Peter Ndomba, amesema nia yao ni kuhakikisha wanaona watanzania wote wanaachana na matumizi ya kuni na mkaa wataki wa kupika.

Amesema sera yao ni kuhakikisha nchi nzima inatambua umuhimu wa kutumia gesi "Hii ni kampeni ya kitaifa ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliizindua kwa lengo la kuhakikisha kwamba miaka 10 ijayo zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi".

"Kuni na mkaa vimekuwa na madhara makubwa ya afya kwa watu, kiuchumi na kijamii, watu wanaugua magonjwa yasiyoeleweka ikiwemo Kansa, mfumo wa kupumua na macho jambo linalosababisha waingie gharama kubwa kujitibia," amesema Ndomba.