Kunenge: Msishangilie Hati safi, mjikite kwenye matumizi yenye tija

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:19 PM Jun 20 2024
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge
Picha: Julieth Mkireri
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema halmashauri za mkoa huo hazitakiwi tena kushangilia kupata Hatisafi badala yake wajikite kwenye matumizi yenye tija.

Kunenge ameyasema hayo alipokuwa katika kikao cha Baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya Mkuranga kujadili hoja za Mkaguzi wa hesabu za Serikali lililofanyika humo.

Akizungumza katika Baraza hilo Kunenge amesema halmashauri za mkoa huo zimekuwa zikipata hati safi kila mara jambo ambalo kwasasa limekuwa la kawaida na wanatakiwa kujikita kwenye matumizi yenye tija kwa kuangalia vipaumbele.

Amesema wananchi wanataka kuona hali halisi kwenye maisha yao ya kila sikuna sio kwenye makaratasi kwa kuandika katika utaratibu wa asilimia.

1

Kunenge amesema kuanzia mwaka ujao kila mkuu wa idara awajibike na hoja zake mwenyewe na kwa utaratibu huo utasaidia kutokuwa na hoja katika vipindi vijavyo.

Kadhalika mkuu huyo wa mkoa ameelekeza halmashauri hiyo kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuongeza umahiri wa kukusanya sambamba na kuwa makini kwenye matumizi kwa kutumia maeneo yenye tija.

Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchata aliipongeza halmashauri hiyo kwa kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato.
2

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir alitoa rai kwa watumishi kuwa waadilifu na kila mkuu wa idara anatakiwa kukaa na wataalamu wake na kujadili mikakati ya kuinua mapato.

Nassir pia alimuaguza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Waziri Kombo kukaa na timu yake kuhakikisha fedha zinazotengwa zinaenda kujibu hoja za wananchi ambao ndio walengwa.
3

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mohamed Mwela amesema Halmashauri hiyo imetokea maagizo yaliyotolewa watayafanyia kazi.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Waziri Kombo alisema hoja zilikuwa 49 na hadi sasa zimefungwa 31 na 18 zilizobaki zinaendelea kufanyiwa kazi.

4