Laini za simu 17,000 za 'tuma kwenye namba hii' zafungiwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:04 AM May 28 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari.
Picha: Maktaba
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema zaidi ya laini za simu 17,300 zimefungiwa kupokea na kutoa mawasiliano kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kujihusisha na uhalifu mtandaoni katika kipindi cha miezi mitatu.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwenendo wa Sekta ya Mawasiliano iliyotolewa na TCRA, matukio ya ulaghai yamepungua kutoka laini 20,939 zilizofungwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka 2023 hadi 17,318 Januari hadi Machi mwaka huu sawa na kupungua kwa asilimia 15.

Akizungumzia mwenendo huo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, alisema kupitia ripoti inaonyesha kuwa hadi kufikia Machi 2024, mikoa ya Rukwa na Morogoro ilikuwa inaongoza kwa matukio ya simu za ulaghai kwa kuwa na theluthi mbili (2/3) ya matukio yote.

Alisema mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Tabora inafuata kwa matukio machache ya ulaghai. Maeneo mengine yalikuwa na matukio machache zaidi ya ulaghai kwenye simu, hasa mikoa ya Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.

Dk. Bakari alisema TCRA imebaini simu za ulaghai zinazoingia nchini na hatua stahiki zinachukuliwa. Idadi ya simu za udanganyifu pia imeendelea kupungua.

"TCRA imesimamia katika kuzuia matumizi ya simu zilizoripotiwa kuibiwa, kupotea au kuharibika pamoja na kuzuia matumizi ya simu zisizokuwa na viwango au za bandia. Usimamizi huu unawezesha kubaini na kufungia namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano zilizonakiliwa (Duplicate IMEIs).

“Namba tambulishi za vifaa vilivyotumika kwenye udanganyifu pamoja na namba tambulishi zilizotolewa taarifa ya kupotea au kuibiwa," alifafanua.

Alisema TCRA imeendelea kuhimiza wananchi kuendelea kuripoti kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) simu zote zenye viashiria vya ulaghai au utapeli kwa kutuma namba husika (za matapeli) kwenda namba 15040 bila malipo.