Majaliwa asema sasa nchi haina mgawo wa umeme

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:13 AM Apr 20 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, serikali imetenga na kutumia zaidi ya Sh. trilioni 8.18 katika sekta ya nishati na kwamba kwa sasa nchini kuna uhakika wa umeme.

Aidha, ameagiza Wizara ya Nishati kusimamia kupunguza au kuondoa kabisa mrundikano wa maombi ya kuunganisha huduma za umeme na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), likomeshe ukiritimba na ucheleweshaji wa huduma hiyo.

Akifunga Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyofanyika viwanja vya Bunge, Majaliwa alisema sekta hiyo inagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania na injini ya uchumi wa taifa ndiyo sababu ya Rais kuipa kipaumbele kwa kutenga fedha nyingi.

“Tunakumbuka miezi michache iliyopita tulikuwa na adha ya mgawo wa umeme hapa nchini. Jana nimemsikia Naibu Waziri Mkuu akitangaza kumalizika kwa mgawo wa umeme kwa nchi nzima. Ninampongeza sana kwa hatua hiyo muhimu. Ninatambua kazi kubwa aliyoifanya ili kuhakikisha utatuzi wa changamoto za upatikanaji wa nishati.

“Niseme tu sasa sekta ya nishati imetulia na Watanzania wanaendelea kupata huduma inayostahili ili kuinua maendeleo na kipato chao,” alisema.

Majaliwa alisema katika sekta ndogo ya umeme, malengo makuu ya serikali ni kuhakikisha uzalishaji wa umeme unafikia megawati 5,000 ifikapo mwaka 2025.

“Kama nilivyotangulia kusema, kazi hiyo inafanyika kwa vitendo ambapo utekelezaji wa miradi ya kuzalishaji umeme ya Bwawa la Julius Nyerere megawati 2,115, umeme jua wa Kishapu Shinyanga megawati 150, Kinyerezi I Extention megawati 185 pamoja na miradi mingine inayoendelea ni kielelezo tosha cha kufikia malengo hayo,” alisema. 

Majaliwa aliwashauri wabunge kufunga mfumo wa gesi katika magari yao ili kuwasaidia kupunguza gharama za mafuta.

Akizungumzia nishati safi, Waziri Mkuu alisema serikali imeandaa mkakati wa kusimamia nishati safi ya kupikia ambao unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni unaolenga ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania waitumie ili kupunguza vifo takribani 33,000 na kuokoa takribani hekta 469,420 za misitu ifikapo 2030.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alisema, “watu wanaamini TANESCO ni wakata umeme sio waleta umeme, na kwamba serikali imedhamiria kuondoa mtazamo huo kwa Watanzania kwa kuimarisha utendaji kazi.”

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alishauri serikali itengeneze gridi ya maji kama ilivyo gridi ya umeme ili kukusanya maji ambayo yanasababisha mafuriko maeneo mbalimbali na kuwa na uhakika wa huduma hiyo.

Awali, akitoa taarifa ya maonesho hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, alisema hoja zilizojitokeza ni za umeme, nishati jadidifu ambapo asilimia 42 zilihusu maunganisho ya umeme kwenye vitongoji huku asilimia 24 ni za mafuta na gesi.