Makamba ataja maeneo ya kuboresha Wizara ya Mambo ya Nje

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:51 PM Apr 22 2024
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ametumia takribani saa moja kuelezea maeneo ambayo yatajajadiliwa katika warsha ya Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani inayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere mjini Kibaha kuanzia leo kitakachodumu mpaka Jumatano.

Katika maelezo hayo, Waziri huyo amewataka washiriki wa warsha hiyo ambao ni Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Mabalozi, Wakuu wa Utawala balozini, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi wa Wizara hiyo kujadili kwa upana maeneo hayo ili Wizara iweze kufikia malengo iliyowekewa na Serikali.

Maeneo aliyoyataja ni pamoja na kuboresha mawasiliano ndani ya Wizara, baina ya Wizara na taasisi nyingine na wadau wake. Amesema hakuna namna Wizara ambayo majukumu yake ni uratibu ikafikia ufanisi unaohitajika bila kuwa na mfumo madhubuti wa mawasiliano.

Amesema eneo lingine ni umuhimu wa Wizara kuweka mfumo madhubuti zaidi wa kufuatilia utekelezaji wa matukio ambayo imekuwa ikiyaratibu tena kwa ufanisi mkubwa. Matukio hayo ni pamoja na masuala yanayoafikiwa katika ziara za viongozi, Mikutano, makongamano ambayo yana faida kubwa kwa nchi kama yatafuatiliwa vyema utekelezaji wake.

ameongeza kuwa kuna umuhimu wa Wizara wa kuweka mfumo wa kuwaongezea maarifa, weledi na ujuzi maafisa wake, hususan katika uandishi na kuzungumza akisisitiza kuwa nchi yetu inasifika na kutangazika kutokana umahiri wa wanadiplomasia wake, na kwamba jambo hiloambalo limekuwa urithi wetu, hivyo lazima liendelezwe kwa kuwapatia watumishi ujuzi unaohitajika.

Suala lingine alilosisitiza ni umuhimu wa kuwa na mfumo wa kuwajibishana akibainisha kuwa mfumo huo utasaidia kuhamasisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika Wizara. 

Pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda heshima na hadhi ya nchi yetu huko Nje. Alisema kuwa kufanikisha hilo ni pamoja na kuwa na mazingira bora ya utendaji kazi huko nje ikiwa ni pamoja na kuwa na vitendea kazi vinavyohitajika.

Amesema Serikali itahakikisha inaboresha mazingira ya kazi ili nchi iendelee kulinda heshima yake iliyojengwa kwa muda mrefu na viongozi waliopita. 

Makamba amewapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya licha ya changamoto wanazokabiliana nazo. Amesema tokea ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa muda wa miezi saba sasa amebaini kuna uwezekano wa kufanya mambo makubwa zaidi na ndiyo moja ya sababu ya kuitisha warsha hiyo ambayo ameitaja kuwa ni ya kubainisha changamoto, kuzitafutia ufumbuzi na kuweka mpango wa utekelezaji wenye tija kwa maslahi ya nchi.