JESHI la polisi mkoani Arusha limetakiwa kutatua changamoto za matukio ya uhalifu, Rushwa na dawa ya kulevya na kuhakikisha yanakuwa ni historia mkoani humo.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda, alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi kilichohusisha uongozi wa Jeshi la Polisi mkoani humo.
Makonda amesema jeshi la polisi linapaswa kufahamu taarifa za uwepo wa wauzaji na watumiaji wa dawa ya kulevya mkoani humo haileti taswira nzuri kwa kuwa mkoa huo unapaswa kuwa kitovu cha kuzungumzwa kwa mazuri kutokana na raslimali zilizopo, hivyo wanaweza kutengeneza hofu kwa baadhi ya wageni kuingia na kufanya biashara.
Amesema vita ya dawa ya kulevya haijawahi kuwa nyepesi, hivyo maafisa wa jeshi la polisi mkoani humo wanatakiwa kujipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda vita hivyo.
Akizungumza masuala ya rushwa, Makonda amewataka askari na maafisa wa polisi mkoani humo kujitengenezea taswira njema kwa jamii kwa kuwa haipendezi na haikubaliki kuona askari mmoja anapokea mlungula ambayo kwa namna moja au nyingine madhara ya tukio hilo yanaathiri jeshi la polisi kwa ujumla.
Makonda amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo,
kuhakikisha anasimamia nidhamu na weledi kwa jicho kali na pale inapotokea askari mmoja, au kituo kimoja kinalalamikiwa kwa rushwa na matendo mengine yasiyofaa hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka, kwa kuwa mafanikio ya mpokea Rushwa ni laana inayoathiri watoto na familia yake kwa ujumla
Amewataka maafisa hao kutambua kuwa wana wajibu wa kutoa huduma nzuri kwa wananchi na matarajio yake ni kuona jeshi la polisi mkoa wa Arusha linakuwa la mfano nchini kwa weledi, nidhamu na uwajibikaji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED