Makonda amlilia Dk. Mpango maboresho ya barabara

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 03:02 PM May 01 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amemuomba Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, kumsaidia kujenga na kurekebisha barabara kwa kuwa uchakavu wake ni mkubwa na kuathiri mwendo wa ukuaji wa utalii.

Makonda ametoa kauli hiyo leo kwenye kilele cha siku ya Wafanyakazi duniani ambayo Kitaifa yanafanyika Mkoani Arusha katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid ambapo mgeni rasmi ni Mpango akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kutokana na wingi wa wageni na watalii wanaofika Mjini Arusha ni muhimu kuweka miundombinu ya barabara katika hali nzuri ili kuendana na hadhi ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro KIA, uwanja unatumika na wageni na Watalii wengi wanaofika Mkoani Arusha kwenye shughuli mbalimbali. 

Aidha, Makonda amesisitiza suala la umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania na kumuahidi Makamu wa Rais kuwa atapambana kulinda na kutetea umoja na mshikamano dhidi ya watu wenye nia ovu.

Makonda amewashukuru wana Arusha na Mikoa jirani kwa kujitokeza kwa wingi kuhudhuria sherehe hizo za Mei Mosi mwaka huu kiasi cha kutokuenea kwenye uwanja wa Michezo Sheikh Amri Abeid na hivyo kulazimu Skrini kubwa kufungwa pembezoni mwa uwanja ili kuruhusu wananchi kufuatilia  kinachoendelea kwenye sherehe hizo za Mei Mosi.