Makonda asubiriwa kwa hamu kuibadilisha Arusha

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 10:18 AM Apr 08 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
PICHA: CCM
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

BAADHI ya wafanyabiashara mkoani hapa wamesema wanamsubiri kwa hamu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kwa ajili ya kuwatatulia kero zao ikiwamo sekta ya utalii kwa madai kuwa wanaonufaika ni wageni.

Vile vile, wanasubiri kufufuliwa kwa viwanda vilivyokufa ambayo vilikuwa vinategemewa na wananchi. 

Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha leo anatarajiwa kukabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake, John Mongela. 

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki na mfanyabiashara Dk. Philemon Mollel, maarufu Monaban amesema kwa sasa changamoto zao zitakwenda kutatuliwa kwa kuwa Makonda ni mchapakazi. 

Amesema Makonda kupelekwa mkoani Arusha ni sawa na kusema kiatu kimempata mvaaji na wana imani matatizo yao yamefika mwisho. 

Mollel amesema wafanyabiashara wanampokea kwa mikono miwili na kumuunga mkono na wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa wamepata sehemu ya kupeleka matatizo yao.

Amesema wafanyabiashara wanafanya kazi kwa kuitegemea serikali na wanahitaji mtu ambaye akipatiwa kero zao zitatatuliwa. 

Kadhalika, amesema Arushakuna viwanda vilikuwa havijafunguliwa na sasa wana imani vinaenda kufunguliwa na fitina zote zilizokuwapo kiboko yao ni Makonda. 

"Hapa Arusha hatuhitaji fitina wala ugomvi, tunahitaji amani ni sehemu ambayo watalii wapo kila siku na Arusha ni lango la mji, pakiwa na amani Tanzania nzima imekuwa na amani na mambo mengi yamekuwa yakifanyika hapa kwa kuwa tumempata Makonda," amesema Mollel. 

Aidha, amesema wataendelea kuviombea vyama vya siasa kuwa na umoja na ushirikiano kwa sababu maandiko yanawataka watu wakae kwa pamoja ili Arusha iwe kitu kimoja na wapate maendeleo na kuishi kwa amani.

Mfanyabiashara Nathan Kimaro, amesema Makonda atakuwa mwarobaini wa kutatua changamoto zao zilizokuwa zikiwasumbua kwa muda mrefu. 

"Mkoa wa Arusha unategemea sekta ya utalii na wanaonufaika sio Watanzania wazawa, tuna makampuni mengi ya ndani lakini wazawa hawajapata mafanikio makubwa kwa kiwango cha utalii tunamuomba Makonda ahakikishe anayanyanyua makampuni ya kitalii ndani ya mkoa huu yaweze kuwa sehemu ya keki ya taifa ya utalii," amesema.

Amesema hata vijana ambao wanawasindikiza watalii hawanufaiki na kazi wanayoifanya na kujikuta wakiendelea kuishi katika mazingira magumu. 

Aidha, amesema jiji la Arusha limekosa mandhari nzuri kama ilivyo ukubwa wa jina lake kwa kuwa bado ni chafu na sekta ya madini haijaweza kunufaisha watu wengi. 

"Uwapo wa thamani ya madini pale Mererani haijaakisi maisha ya Mtanzania mmoja mmoja kwa hapa Arusha sasa itakuwa vizuri soko letu la madini liwe soko la madini kimataifa wazungu waje na watu wengine ili Tanzanite iweze kuuzwa na kutusaidia sisi," amesema Kimaro. 

Kimaro amesema sekta ya makazi ya kujivinjari na nyumba bado imekuwa ni changamoto kama alivyoeleza Rais Samia ni kweli ndani ya mkoa wa Arusha wakija watalii 1,000 hakuna pa kuwalaza sasa ni wakati wa Makonda kuwaleta wawekezaji kuja kujenga magorofa ya hoteli.

Amesema changamoto nyingine ni kukosekana kwa mipango mini katika jiji la Arusha kwa sababu watu wameanza kujenga kiholela wakati ni jiji la kitalii. 

Naye mfanyabiashara anayechoma nyama katika eneo la Kwa Mrombo, Kata ya Murieti, Mwijuma Mbaruku, amesema wanafanya biashara zao katika mazingira magumu licha ya kulipa ushuru bila kufanyiwa maboresho kwa muda mrefu.

"Tunaomba watuwekee mifereji ya kupitisha maji haya mazingira hayavutii tuna jina kubwa na kila anayefika Arusha lazima aje kula nyama hapa kwa Mrombo hadi wazungu wanakuja ukiangalia haya mazingira hayaridhishi watuboreshee ili wanaokuja wafurahie mazingira," amesema.