Makonda azindua magari ya uokoaji na zimamoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:58 PM May 20 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda,akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Zimamoto Mkoa Arusha.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda,akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Zimamoto Mkoa Arusha.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kushirikiana na Mamlaka ya Maji katika kuvitambua, kuviendeleza na kuvitunza visima maalum vya maji vilivyokusudiwa kutumika kwenye uzimaji wa moto.

Makonda agizo hilo leo kwenye Kituo Kikuu cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha wakati wa uzinduzi wa magari mawili (2) mapya ya zimamoto na uokoaji yaliyotolewa na serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan yenye thamani ya Sh. bilioni mbili.

Makonda amesema amebaini visima vingi vilivyopo mkoani Arusha vimetelekezwa na kutoendelezwa na kulitaka jeshi la zimamoto na uokoaji kuvihuisha, kuhakikisha vinatambulika na vinakuwa tayari muda wote kwa matumizi yaliyokusudiwa na serikali katika kuhudumia wananchi kwenye uokozi.

Aidha, Makonda ameitaka Mamlaka ya maji mkoani Arusha wanashirikiana na Jeshi hilo la zimamoto na uokoaji katika kuongeza visima vya maji kwenye maeneo ya pembezoni mwa mji ambapo hakuna visima hivyo vya kutumika kwenye matukio ya uzimaji wa moto.

Makonda amewaomba wananchi wa mkoa wa Arusha kuzingatia mipango mizuri ya ujenzi wa nyumba na kuhakikisha wanatenga maeneo ya barabara za kuingia kwenye maeneo yao pindi ajali mbalimbali zinapotokea.

Aidha, Makonda amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia magari hayo.