Makonda: Nipo tayari kupoteza chochote nilichonacho

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 02:23 PM May 08 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewaambia wananchi wa mkoa huo kwamba yupo tayari kupoteza chochote alichonacho ili mwananchi mmoja wa Arusha aweze kupata haki yake na kunufaika na cheo chake.

Makonda ameyasema hayo leo wakati akizungumza na  wananchi waliojitokeza kwenye kliniki ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Amesema hawezi kukaa kwenye kiti cha mkuu wa mkoa ilihali wananchi anaowaongoza wakiteseka na changamoto mbalimbali ambazo zipo ndani ya mamlaka yake ya uongozi.

Aidha, Makonda amewataka wananchi hao kung'ang'ana kudai haki yao wasiogope kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa wanasheria bingwa kutoka ofisi zaidi ya 75 za mawakili ili kuwasikiliza na  kuwapa misaada ya kisheria.

Makonda amesema hatokubali kuendelea kuona vilio vya wana Arusha waliokata tamaa kutokana na kutosikilizwa kero zao na kutatuliwa akiahidi kuijenga heshima yake kwa kurejesha haki kwa wananchi wa Arusha walionyang'anywa haki zao.