Makonda: Sitishwi na kelele za mitandaoni

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 10:01 AM May 28 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewajibu wanaomshambulia katika mitandao ya kijamii, akisema hatishwi na kauli hizo, kwamba ni sawa wanabembeleza na kumwongezea nguvu katika utendaji kazi wake.

Alitoa kauli hiyo jana akiwa kwenye ziara Wilaya ya Monduli mkoani Arusha kwa ajili ya ukaguzi wa miradi na kutatua kero za wananchi.

“Nasikia kuna watu wanahangaika mitandaoni, ni kama wananipigia mdundo yaani na umri huu nitishike na kauli za watu? Ulishawahi kwenda kwenye chumba cha massage halafu ukawekewa kale kamziki inakuwa kama rhythm. Sasa mimi ndio ninavyojisikia,” alisema Makonda na kuongeza:

“Wanavyoendelea kutoa hizo kauli mimi nasikia hiyo hali ya kunibembeleza ikiniambia nenda Makonda endelea na leo (jana) nipo Monduli kuwapiga spana wavivu wote hatuwezi kwenda hivyo.”

Aidha, alimwomba Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, kusimamia miradi na asisite kuwachukulia hatua wanaohusika na ubadhirifu.

“Mfahamu miradi isipotekelezwa ndani ya muda hawa makandarasi kuna namna wanaongeza gharama ambayo ni maumivu kwa mwananchi yaani mwananchi ateseke miaka yote tumepewa upendeleo wa shule ya wasichana ili kuondoa mimba za utotoni ipo Longido, ili mradi ukamilike tunatakiwa kuwa na fedha ya ziada inatoka wapi?,” alihoji Makonda.

Makonda amesema: “Ukishafika Monduli upande mmoja una Edward Sokoine na upande wa pili ni  kuna Edward Lowassa halafu unakuwa muoga, ninaomba mwendelee kunipigia mdundo…wale mnaotoa kauli mnanisaidia kufanya kazi kwa molari kubwa.”

Amesema kuna siku alieleza umoja wa waovu, wala rushwa na wazembe ni mkubwa sana.

Makonda alisema: “Ukitaka kujua kama upo mguse mvivu mmoja utaona wavivu wote wanajitokeza au mguse mla rushwa mmoja wala rushwa wote wataibuka.”

Aliongeza: “Nawaambia tena nitawapiga spana na mnavyojitokeza tunapata nafasi ya kujua kumbe naye huyu yumo…alizalilishwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, mwanadiplomasia namba moja, mama mwenye familia katukanwa asubuhi hadi asubuhi sijasikia kauli ya mtu yoyote sisi wanaume tulijitokeza kumpigania yule mama.”

Alisema: “Leo mzembe mmoja mla rushwa mmoja mnapiga kelele huko ebooo!” Amesema Makonda.

Aidha, Makonda alisema wapo watumishi wilayani Monduli waliokusanya fedha za ushuru na hazijulikani zilipokwenda akisema atamalizana nao.

Alisema tayari amemwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha kama mtumishi hawezi kufanya kazi inavyotakiwa aandike barua ya kuhama, watamsaidia aondoke.

Makonda alisema: “Mkuu wa Wilaya simamia bila kutetereka na bahati nzuri bosi wako ni mimi kila mmoja ataripoti kwa bosi wake. Tukicheka cheka hivi itafikia hatua kuna miradi ambayo itakuwa haiendi mtumishi yoyote hakikisha anakupa matokeo.”