Makonda: Wateja wanalalamika kucheleweshewa huduma Mpakani

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 07:55 PM Apr 19 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda,.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewataka watumishi wa serikali wanaofanya kazi kwenye mpaka wa Namanga unaotenganisha Tanzania na Kenya kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania na kufanya kazi kwa nidhamu na weledi wanapohudumia wateja wao.

Makonda ameyasema hayo leo ulipofanya ziara kwenye mpaka huo kwa ajili ya kujionea shughuli zinazofanyika, changamoto na hatua zinazochukuliwa.

Amesema  kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja wanaofika kwenye mpaka kwa ajili ya kupata huduma wakilalamikia kuchukua muda mrefu kufanyiwa uhakiki jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linadhoofisha ufanisi.

Makonda amesema ili kuzuia jambo hilo ni vyema watumishi wa idara mbalimbali kwenye mpaka huo wakajipanga kikamilifu kuhakikisha wateja wanaofika kupata huduma kwa haraka.

Aidha,  Makonda ametoa  wito kwa watumishi hao kuhakikisha unawekwa mfumo utakaoruhusu mteja akifika kwenye eneo moja awe anaonekana kwenye maeneo yote na  kuhudumiwa bila hata ya kuonana na Ofisa wa mamlaka, idara au taasisi husika kufanya hivyo si tu kutaharakisha utoaji wa huduma  kunapunguza vishawishi vya kutokea kwa Rushwa.

"Taswira ya kwanza ya mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla inaanzia kwao hivyo, wanapaswa kujuwa kuwa pale wanapotoa huduma zisizoridhisha zinazowakwaza wateja wafahamu wazi kuwa ujumbe  huo hasi unaweza kuathiri Taifa endapo wahusika watautangaza kwa wengine jambo ambalo halikubaliki,"amesema Makonda.