MAPENDEKEZO BAJETI... Macho, masikio makao makuu Dodoma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:46 AM Jun 13 2024
Macho, masikio makao makuu Dodoma.
Picha: Mtandao
Macho, masikio makao makuu Dodoma.

MACHO na masikio ya Watanzania leo yanaelekezwa Makao Makuu ya nchi Dodoma wakati Mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 yakisomwa, huku matarajio yakiwa ni kutoa kipaumbele kwenye mahitaji muhimu kama maji, umeme, elimu na miundombinu.

Machi 11, mwaka huu, serikali ilipendekeza ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2024/25 kuwa ni Sh. trilioni 49.34, sawa na ongezeko la asilimia 11.2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh. trilioni 44.3, huku asilimia 70.1 ikitarajiwa kutoka katika mapato ya ndani.

Akiwasilisha mapendekezo hayo kwenye Kamati ya Bunge zima, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema kati ya mapato hayo, Sh. trilioni 29.9 yanatarajiwa kuwa ni makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema pia mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na wizara, taasisi na idara zinazojitegemea, yanatarajiwa kuwa ni Sh. trilioni 3.4 na mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sh. trilioni 1,344.1.

"Sehemu kubwa ya bajeti asilimia 70.1 itagharamiwa na mapato ya ndani ambayo yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 10.0 mwaka 2024/25," alisema Nchemba.

MIKOPO YA ELIMU

Katika mwaka 2024/25, Mwigulu alisema kati ya Sh. trilioni 33.55 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 15.78 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na ongezeko la asilimia 3.8.

Pia, alisema fedha za maendeleo zinajumuisha ruzuku ya maendeleo ya Sh. trilioni 1.23 kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya kati na ya juu pamoja na programu ya elimu msingi na sekondari bila ada.

Aidha, alisema utengaji wa fedha za maendeleo umezingatia miradi inayoendelea ikiwamo ya kimkakati na ya kielelezo pamoja na utekelezaji wa miradi kupitia utaratibu wa ushirikiano na sekta binafsi (PPP) ili kuipunguzia serikali mzigo wa kugharamia miradi ya maendeleo kwa utaratibu uliozoeleka.

Ili kufikia malengo na shabaha za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25, Mwigulu alisema sera za mapato na hatua za kiutawala kwa mwaka 2024/25 zitalenga kuongeza makusanyo ya mapato kwa kuendelea, kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Ikiwa ni pamoja na kuwianisha, kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada zinazoonekana kuwa kero, kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari, kuongeza wigo wa kodi.

Pia, kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; na kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato, hususani kodi ya ardhi na pango.

Katika mwaka 2024/25, alisema serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria ya bajeti, sura 439, Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 na Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 ili kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kugharamia mahitaji yasiyoepukika ikijumuisha mishahara na deni la serikali.

Kadhalika, alisema serikali itaendelea kugharamia matumizi ya maendeleo yenye vyanzo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo maalum yenye maslahi mapana kwa taifa kama vile Mfuko wa Barabara, Mfuko wa Reli, Mfuko wa Umeme Vijijini na Mfuko wa Maji na Wakala wa Maji Vijijini.

Vile vile, alisema serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai pamoja na kufanya maboresho katika mfumo wa ununuzi wa umma ili kuhakikisha unakuwa wenye tija na kuendana na thamani ya fedha.

Mwanadiplomasia na mchambuzi wa siasa, Hamduni Maliseli, alisema kuwa bajeti ya mwaka huu itakuwa ya kihistoria kwa kuwa inaiingiza nchi katika uchumi wenye nguvu unaoonekana katika wingi wa fedha zinazoingizwa katika wizara mbalimbali ili kuunga mkono utendaji wa serikali.

Alisema bajeti hiyo inaakisi matarajio ya Watanzania kuwa inayotegemea mapato ya ndani kwa zaidi ya asilimia 70 na kwamba ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa fedha hizo zinafanya kazi kama zitakavyelekezwa.

Alisema bajeti hiyo ikitekelezwa kama ilivyokusudiwa italeta mapinduzi katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, elimu na uwekezaji hali itakayochangia kukuza kipato cha wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, CPA David Mwakapala alisema bajeti hiyo imejikita katika kuimarisha miradi ya maendeleo hali inayoonyesha dhima ya serikali ya kumkomboa mwananchi katika kadhia mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, Visent Mbogo, alisema kuwa matarajio ya bajeti hiyo ni kuwagusa wananchi wa kipato cha chini wakiwamo wakulima wadogo, wafanyabiashara wa chakula na viwanda vidogo vinavyoajiri vijana.

Mbunge wa Viti Maalumu Tuza Malapo anasema ni matarajio yake kuwa yale mambo yote waliyoshauri kwenye mapato, matumizi, elimu, mifugo uvuvi na ukusanywaji wa kodi yatakwenda kufanyiwa kazi na kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi.

Mkazi wa Korogwe vijijini, Janeth Msofe, alisema anatarajia bajeti hiyo kutoa kipaumbele Wizara ya Afya kwa kuwa inapitia changamoto nyingi hasa maeneo ya vijijini ambako bado kinamama wanatembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya ikiwamo kujifungua.

Mkazi wa Mwanza Mjini, Innocent Mtemi, alipendekeza bajeti hiyo itoe kipaumbele miradi endelevu kama vile treni ya umeme ya GSR na bandari kwa sababu vina mwingiliano wa moja kwa moja na shughuli za kiuchumi za wananchi.

*Imeandikwa na Jenifer Gilla (DAR) na Paul Mabeja, (DODOMA)