Mawakili wajipanga kutumia ujuzi wao kutatua kero Njombe

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 08:54 PM May 27 2024
Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo ( Tanzania Law School), Dk. Clement Mashamba, akizungumza na waandishi wa habari mjini Njombe.
Picha: Elizabeth John
Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo ( Tanzania Law School), Dk. Clement Mashamba, akizungumza na waandishi wa habari mjini Njombe.

CHAMA cha Mawakili wa Serikali Tanzania kimewaahidi wananchi mkoani Njombe kutumia ujuzi wao wa sheria kutatua kero mbalimbali watakazoziwasilisha kwenye kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.

Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Amedeus Shayo wakati uzinduzi wa kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria (Mama Samia Legal Aid) iliyofanyika halmashauri ya Mji ya Njombe.

“Mkoa wa Njombe ni mkoa ambao umefikiwa na kampeni ya mama Samia, sasa wananchi wa Njombe wanamatatizo mtambuka sisi tunaleta Njombe taaluma yetu ya wanasheria na tunawakaribisha wananjombe kutoka wilaya zote na tutatumia ujuzi wetu wa sheria,” amesema Shayo.

Naye Kaimu Naibu Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo Tanzania (Law School), Dk. Clement Mashamba amesema wamefika Njombe kushirikiana na wadau wengine ili kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria.

“Sisi ni Taasisi ya mafunzo ya kisheria hivyo kutoa msaada wa kisheria ni sehemu ya kazi yetu lakini pia kwenye taasisi yetu tuna kituo cha msaada wa kisheria ambacho kinatoa huduma hizi kwa wananchi,” amesema Dk. Mshamba.

Aidha Dk. Mashamba amebainisha kuwa taasisi hiyo inatoa kozi ya Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) kwa ngazi ya Cheti na Diploma ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wataalamu wa masuala ya sheria wanaongezeka na huduma zinasogea karibu zaidi katika maeneo mbalimbali nchini.