Mbaroni madai kusafirisha nje punda 46 kinyume cha taratibu

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 05:53 AM May 26 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Punda

JESHI la Polisi Kikosi cha Kupambana na Kuzuia Wizi wa Mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Longido mkoani Arusha wamekamata watuhumiwa wanne pamoja na punda 46 waliokuwa wakisafirishwa kinyume na taratibu kwenda nje ya nchi.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi hicho nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Simon Pasua, alisema watu hao wamekamatwa kwa kushirikiana na wananchi pamoja wizara hiyo.

Kamanda Pasua alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, huku majina yao yakihifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

Alisema tayari serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilishatoa maelekezo kuhusu katazo la kusafirisha punda na mazao yake kutokana na kupungua kwa idadi yao.

SACP Passua aliweka wazi kuwa, jeshi hilo litaendelea kuwakamata wale wote watakaobainika kuhusika na usafirishaji wa wanyama hao kwenda nje ya nchi.