Mbowe, Lissu kunguruma jukwaa moja wiki tatu wakitumia helikopta

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:19 AM Jun 21 2024
Mbowe, Lissu kunguruma jukwaa  moja wiki tatu wakitumia helikopta.
Picha: Nipashe Digital
Mbowe, Lissu kunguruma jukwaa moja wiki tatu wakitumia helikopta.

MKUU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); Freeman Mbowe na Makamu wake, Tundu Lissu, kuanzia kesho wataanza mikutano mfululizo wiki tatu katika mikoa ya Kaskazini wakitumia helikopta.

Ni ziara waliyoibatiza kijeshi ‘Operesheni GF’ itakayoongozwa na mwenyeji wao, Godblesas Lema, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, taarifa iliyotolewa jana na CHADEMA inaeleza.

Ziara hiyo inatarajiwa kugusa majimbo zaidi ya 30, ikipewa jina la 'Operesheni GF'. Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara.

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema jana kuwa operesheni hiyo inalenga kujenga chama katika mikoa hiyo.

Alisema kuwa katika majimbo ya Ngorongoro na Karatu kutafanyika mikutano mitano, kila jimbo na viongozi wote wakuu, Mbowe na Lissu wanatarajia kunguruma kwenye jukwaa moja.

"Kwa majimbo ya Ngorongoro na Karatu tunatarajia kufanya mikutano mitano katika majimbo hayo, na kwa upekee Mwenyekiti wa Taifa (Mbowe) atashirikiana na Makamu Mwenyekiti Lissu," alisema Golugwa.

Katibu huyo alisema operesheni hiyo inatarajiwa kuanzia Jimbo la Karatu, mkoani Arusha, na kwamba katika majimbo mengine, mikutano hiyo itaongozwa na Mbowe na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

Golugwa alisema kwa sasa wanaendelea kukamilisha maandalizi ya operesheni hiyo.

"Kaulimbiu yetu tunataka kuonesha Watanzania kwa ujumla kwamba tuna watu, tuna Mungu, tuna nguvu. Hiyo ndiyo fahari yetu na uimara wetu Kanda ya Kaskazini ambayo ni ngome ya CHADEMA.

"Tunaendelea na maandalizi ikiwamo kupeleka barua ya vibali vya mkutano, ndege kuruka na masuala mengine," Golugwa alisema.

Katibu huyo alisema operesheni hiyo inafanyika baada ya kumaliza vikao vya mashauriano ndani ya chama vilivyofanyika katika mikoa hiyo ya Kanda ya Kaskazini.

Hii ni operesheni ya kwanza ambayo ni maalum kwa ajili ya kujenga chama hicho, ukiacha maandamano ambayo kilifanya mfululizo yaliyolenga kudai haki katika mambo kadhaa ikiwamo upatikanaji Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na mabadiliko ya sheria mpya za uchaguzi.

Maandamano hayo yalifanywa na chama hicho katika majiji na miji mikubwa nchini, awamu hii polisi wakiimarisha ulinzi kwa waandamanaji. Si kuwapiga mabomu ya machozi ilivyokuwa imezoeleka zamani.