Mbunge adai Dk. Salmin anaishi mazingira magumu

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 10:51 AM Apr 20 2024
 Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma.
Picha: Maktaba
Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma.

MBUNGE wa Baraza la Wawakilishi, Suleiman Haroub Suleiman amesema Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, nyumba yake inakabiliwa na mmonyoko wa udongo kutokana na kuwa karibu na bahari.

Akiuliza swali bungeni jana, Suleiman alisema kuna baadhi ya viongozi ambao walitumikia Serikali ya Tanzania akiwamo Dk. Salmin, ambaye anaishi katika mazingira magumu.

Alihoji kama serikali ipo tayari kushirikiana na viongozi wa kamati ya Baraza Kuu la Wawakilishi Zanzibar ili kutatua hali hiyo.

“Pia kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kutunzwa, lakini hadi sasa yako katika hali hatarishi ikiwamo shule aliyosoma Karume,” alisema.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo alisema ofisi yake inashirikiana vizuri na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar wanalichukua suala hilo ili kujadili namna ya kuboresha maeneo hayo.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alihoji serikali ina mpango gani wa kuwaenzi na kuwatunza waasisi wa Muungano.

Dk. Jafo alisema serikali imekuwa na utaratibu wa kuwatunza, kuzitembelea na kuzifariji familia za waasisi wa taifa kama njia mojawapo ya kutambua mchango wa waasisi wa Muungano.

Aidha, alisema serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kila mwaka kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafanyika.