Mchechu aja na undani kauli ya Samia PSSSF

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:38 AM Jun 13 2024
Msiajli wa Hazina, Nehemiah Mchechu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Msiajli wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, hayakuwa katika kikokotoo ingawa yakifanyiwa kazi kwa kina na kuwa na matokeo chanya, yana nafasi ya kuleta ahueni katika jambo hilo.

Mchechu aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) baada ya hafla ya taasisi na mashirika ya umma kutoa gawio na michango kwa serikali.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Samia alipokea gawio na michango kutoka kwa mashirika 145 yenye thamani ya Sh. bilioni 637.12, zikijumuisha gawio la Sh. bilioni 278.869 kutoka mashirika ya biashara na michango Sh. bilioni 358.254 kutoka taasisi zingine.

Rais Samia aliweka wazi kwamba kuna mashirika ambayo hesabu zake zinachechemea, lakini yana orodha ya miradi mingi yaliyoandaa kutekeleza, akiutaja Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) hauko vizuri.

Kutokana na hilo, Rais Samia alimweleza Msajili wa Hazina kwamba ana kazi na kumwagiza akasimamie mashirika ili wafanyakazi wakistaafu wapate fedha zao kwa wakati bila kusubiri kama walivyokubaliana kisheria.

Alipoulizwa wafanyakazi watarajie nini baada ya maagizo hayo ya Rais hasa suala la kikokotoo, Mchechu alisema maagizo ya Rais hayakuwa kwenye suala hilo.

“Lakini maagizo yake tukiyafanyia kazi kwa kina yakiwa na matokeo chanja yana nafasi ya kuleta ahueni katika kikokotoo ambacho ndio maslahi makubwa ya wafanyakazi waliowekeza akiba yao huko ili wakistaafu wapate maisha bora,” alisema.

Mchechu alisema watu wanapokatwa fedha zao zinakwenda kwenye uzalishaji wenye tija ili kuwa na kiwango au ongezeko la mtaji kilichowekwa kuwasaidia wao na wengine wanaokuja kulipwa kilicho bora.

Alisema mapato mazuri yanatoka kwenye miradi mbalimbali au uwekezaji ambao taasisi hizo za pensheni zinakwenda kuwekeza kwenye miradi ambayo ipo katika uwekezaji wa hisa, hati miliki, dhamana za serikali ambazo zinaweza kuleta fedha.

“Ukiangalia uwekezaji uliofanywa na mifuko pensheni kulikuwa inayokwenda kwenye miliki ambapo kuna vitu au miradi mingine ambayo haikuwekwa vizuri, mapato si mazuri au inawezekana mipango ilikuwa mizuri wakati wa andiko la utekelezaji, lakini hawakusimamia vizuri, au mipango iliandikwa vizuri, lakini usimamizi na uadilifu haukuwa vizuri,” alisema.

Kutokana na hayo, Mchechu alisema wanakwenda kufanya mambo mawili, kwanza kwa kutambua kuwa Rais ni taasisi hivyo wanakwenda kutekeleza maagizo aliyotoa.

Kadhalika, alisema kwa nafasi aliyo nayo ni moja wapo ya kazi ya msajili pale anapoona kuna changamoto au kuna kitu hakijakaa vizuri, sheria inamruhusu kuunda kamati, kuunda tume ya kuchunguza, kuomba nyaraka zozote na hata kuzuia matumizi fulani yanayofanyika.

Mchechu alisisitiza kwamba, katika maboresho wanayokwenda kufanya yatafanya ofisi hiyo kukalia vizuri kazi zake.