Mhariri Mtendaji wa Nipashe ashinda tuzo kimataifa uongozi katika habari

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 03:49 PM May 15 2024
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Beatrice Bandawe.

MHARIRI Mtendaji wa Gazeti la Nipashe, Beatrice Bandawe, ametangazwa kuwa mshindi wa tunzo ya Mwanamke Kiongozi katika Chombo cha Habari (2024 Women In News Laureate Leadership Awards), iliyotolewa na Umoja wa Wachapishaji wa Magazeti Duniani (WAN-IFRA).

Akitangaza washindi wa tunzo hiyo kwa mwaka huu, Melanie Walker, Mkurugenzi Mtendaji wa WAN-IFRA anayeshughulikia Maendeleo ya Vyombo vya Habari na Programu ya Wanawake Katika Habari (Women in News), amesema tunzo hiyo hutolewa kwa wanawake viongozi ndani ya vyumba vya habari waliotoa mchango wa kipekee kwenye sekta na uhuru wa habari, usawa wa kijinsia na kujenga kizazi kijacho cha viongozi. 

Amesema Beatrice kwa zaidi ya miaka 25 katika tasnia ya Habari, ameongoza jitihada katika kupinga ukatili wa kijinsia kupitia vyombo vya Habari, hivyo kutoa mchango makini ulioleta mabadiliko.

Akizungumza katika mahojiano maalum kuhusu tunzo hiyo, Bandawe ambaye amekuwa kwenye taaluma ya habari kwa zaidi ya miaka 30, amesema amepokea kwa furaha kwa sababu ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupokea baada ya nchi za ukanda wa Afrika za Kenya, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Botswana.

“Najisikia faraja kubwa sana kwanza Kampuni ya The Guardian Limited iliniamini kwa kunipa uongozi, nimejitahidi kwa uwezo wangu hadi nimetambuliwa kimataifa, nilichokifanya ni mchango wangu kama kiongozi kuhakikisha maudhui ya taarifa zetu yanazingatia usawa wa kijinsia.

“Mara nyingi habari tunazochapisha hazitoi fursa ya sauti nyingine kusikika, lakini tumeweka utaratibu maalum kwenye chombo chetu kwamba habari zote lazima ziwe jumuishi ili matatizo ya jamii yaweze kufanyiwa kazi,” amesema.

Aidha, ameulizwa ni mambo gani anafikiri yamemfanya awe mshindi, amesema: “Kama kiongozi si kazi yako kuwapangia kazi tu unaowasimamia bali uwaongoze ili nao waje kuwa viongozi kwenye vyombo vya habari. Kuna ombwe kwenye vyumbo vya habari kuwa na viongozi wanawake kwani wengi ni wanaume,” amesema.

Kutokana na tunzo hiyo, amewataka wanawake na wasichana walioko kwenye uandishi wa habari kutokubali kukatishwa 

tamaa na mazingira au maneno kwa kuwa unapokuwa kwenye uongozi kuna mambo mengi.

“Unapokuwa kwenye ngazi ya juu unaweza kukatishwa tamaa. Utaambiwa huna uwezo, hufai kuongoza. Hivyo vyote visikufanye upoteze mwelekeo wa kufanya kazi kwa bidii. Wako watakuona na wataona mafanikio yako, lakini ukikata tamaa wanaokuangalia nao watakata tamaa wataona kuna ugumu huwezi kutoboa, hivyo hutasaidia wanawake kuwa viongozi,” amesema.

Kuhusu nyakati ngumu amewahi kuzipitia kwenye uongozi na aliwezaje kuvuka salama, amesema; ”Ni siku nilipoteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji kwa sababu nilipokea uteuzi wakati watangulizi wangu hawakuwa wameondoka vizuri. 

“Ilikuwa tofauti na vyeo nilivyopewa huko nyuma unafurahia kupata nafasi ya juu. Niliona nimebeba mzigo mkubwa, lakini nilisimamia misingi ya kazi tangu 2018 hadi sasa niko kwenye nafasi hii.

“Wakati mgumu ni pale ambapo unatoa habari alafu inakuwa haijazipendeza mamlaka. Unaitwa unahojiwa, inakuumiza na kukuweka katika wakati mgumu. Lakini kama unasimamia misingi ya kazi, haiwezi kukusumbua kwa kuwa utajitetea na maisha yataendelea.”

Bandawe amesema ushindi huo si wake peke yake bali wa timu nzima ya The Guardian ambayo imempa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yake kwa kuwa hafanyi kazi hizo pekee yake.

“Naipongeza timu yangu wamenipa ushirikiano mkubwa. Tunasikilizana, nasikiliza mawazo yao na nimekuwa nikishirikiana nao kwenye mambo ya kazi na nje ya kazi,” amesema.

Alama anazoziona kwenye taaluma ya habari tangu aingie, amesema: Ninazoziona ni uchapakazi, sijisifii ila nikipewa kazi naifanya kwa uwezo wangu wote. Hii imetoa nafasi kwa wenzangu wote walio chini yangu na ushirikiano na wenzangu sehemu ya kazi na nje ya kazi. Imesaidia sana kuweka ukaribu, mtu hafikiri mara mbili kunifikia na kuomba ushauri na kueleza jambo lake.”

Hata hivyo, amesema tunzo hiyo ni kwa ajili ya wanawake walioko kwenye vyumba vya habari kwa sababu ya uchache wao na lengo si wanawake wawe bora zaidi ya wanaume bali kuwe na usawa na ujumuishi ili sauti zote zisikike katika jamii.

Bandawe amewashauri wamiliki wa vyombo vya habari wazingatie usawa wa kijinsia na si kuangalia wingi wa wanawake lakini na uwezo wao kama ilivyoainishwa katika Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG) ya 50 kwa 50.

“Ni lazima tuangalie wanawake walioko kwenye vyombo vya habari. Kampuni ya IPP Media ni mfano mzuri kwa sababu viongozi wake wengi ni wanawake. Kuanzia ITV, The Guardian Limited na EATV kuna wanawake ngazi ya uamuzi na hiyo inasaidia kuongeza ujumuyishi,” amesema.

Aidha, amewashauri wanawake na wasichana walioko kwenye taaluma ya habari kuendelea kufanya kazi kwa bidi kwa kuwa ni fani nzuri inayowakutanisha na watu wengi, kusafiri sehemu tofauti ndani na nje ya nchi ikiwamo kujifunza mambo mengi. Kwa mantiki hiyo, alisema ni muhimu wazazi kuruhusu watoto wao kusoma fani hiyo.

SAFARI YAKE

Bandawe aliingia katika fani ya habari akiwa mwandishi, baadaye mwandishi mwandamizi, Mhariri wa Habari, Mhariri wa Habari za mikoa, Mhariri Weekend na sasa ni Mhariri Mtendaji.

Tuzo ya 2024 Women in News Laureate Leadership Award imetolewa kwa wanawake viongozi ndani ya vyombo vya habari katika ukanda wa Afrika, Asia na Uarabuni.

Washindi wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa AJ+, Dima Khatib nchini Palestine/Syria na Mkurugenzi na Mhariri Mkuu, Nan Paw Gay wa Karen Information Center, Myanmar.

“Huu ni ushindi wa kupigiwa mfano kwa viongozi walionyesha mfano na kujitoa kwa ubora wa uandishi wa habari, kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine na kuleta mabadiliko chanya kwenye nchi zao na zaidi,” alisema Vincent Peyrègne, Mtendaji Mkuu wa WAN-IFRA. 

“Tunajivunia mafanikio haya makubwa na ni heshima kwa waandishi wa habari ambao wametoa uongozi bora na uvumilivu hasa kwa wakati huu ambao vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto nyingi,” alisema.

Bandawe, Khatib and Paw Gay watatambuliwa kwenye Kongamano la Dunia la WAN-IFRA (World News Media Congress), litakalofanyika Copenhagen, Denmark kuanzia Mei 27-29, mwaka huu.