MORUWASA yapewa mwezi kunywesha maji watu 35000 Moro

By Christina Haule , Nipashe
Published at 09:11 PM May 27 2024
Naibu Waziri wa Maji Kundo Mathew akizungumza na waandishi wa Habari akiwa jirani na tanki la maji (halipo pichani) la Mguruwandege lililopo kata ya Kihonda mkoani Morogoro.
Picha: Christina Haule
Naibu Waziri wa Maji Kundo Mathew akizungumza na waandishi wa Habari akiwa jirani na tanki la maji (halipo pichani) la Mguruwandege lililopo kata ya Kihonda mkoani Morogoro.

SERIKALI imeipa mwezi mmoja Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira mkoani hapa (MORUWASA) ili kuharakisha ukamilishaji na utekelezaji wa huduma za maji kutoka kituo cha Mizani hadi kwenye tanki la Mguruwandege na kusaidia wakazi 35,000 wenye uhitaji huduma hiyo.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amesema hayo wakati akiwa kwenye ziara ya kutembelea vyanzo va maji mkoani Morogoro ambapo amesema ifikapo juni 30 mitambo hiyo inapaswa kuwa imeanza kufanya kazi ya kusukuma maji ili kulisha wakazi hao na kutimiza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“hakikisheni, kama mlikuwa mnafanya kazi kwa masaa 20 basi fikisheni masaa 24, kama mlifanya kazi kwa siku 5 basi fikisheni siku zote 7, hakuna kulala mpaka kieleweke, kazi ikamilike sababu muda nimchache, miradi mingi bado ina changamoto na muda hautusubiri, napenda nione matokeo ya hii kazi” anasema.

Naibu Waziri Mathew ameitaka MORUWASA kuongeza mtandao wa mabomba ili kuhakikisha wateja wanapata maji kwa haraka huku watu wakiunganishiwa maji kwa siku saba tu mara baada ya kupeleka maombi.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutambua umuhimu wa uwepo wa miundombinu ya maji kwa kushirikiana kuilinda ili iweze kutoa maji safi na salama na kuwaepusha na magonjwa yanayoweza kuwakuta wakitumia maji yasiyo salama.

Naye Mkurugenzi wa MORUWASA Mhandisi Tamimu Katakweba amesema tanki la Mguruwandege linauwezo wa kubeba maji yenye ujazo wa lita milioni 2 ambapo licha ya kukabiliwa na changamoto ya mafuriko wanatarajia kukamilisha mradi huo mapema na kuwafikia walengwa.