Msigwa, Sugu rasmi Nyasa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:13 AM May 18 2024
news
PICHA: MTANDAO
Joseph Mbilinyi (Sugu) (kulia) na Peter Msigwa.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetoa baraka kwa Joseph Mbilinyi (Sugu) na Peter Msigwa, kupambana kwenye sanduku la kura katika uchaguzi wa mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Nyasa.

Awali, kulikuwa na tetesi kwamba huenda mmojawapo 'angekatwa' baada ya usaili uliofanywa na Kamati Kuu uliofanyika kwa siku nne kuanzia Mei 11, mwaka huu.

Jana, chama hicho kilitoa orodha ya majina ya walioteuliwa kwenda kupambana kwenye sanduku la kura katika kanda zao, huku Sugu na Mchungaji Msigwa ambao wote waliwahi kuwa wabunge, yakipenya.

Kanda hiyo ndiyo imeonekana kuwa na ushindani mkubwa kuliko kanda zingine na kumekuwa na kupigana 'vikumbo' vya hapa na pale miongoni mwa vigogo hao machachari wa CHADEMA pamoja na wafuasi wanaowaunga mkono kila upande ukitumia mbinu kujigamba.

Walioteuliwa  kugombea katika kanda zingine ni Hezekiah Wenje ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Nyamagana na John Pambalu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA).

Katika orodha hiyo ya wagombea iliyotolewa jana, wamo baadhi ya waliokatwa akiwamo Emmanuel Ntobi, aliyekuwa akiwamia uenyekiti Kanda ya Serengeti, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Shinyanga na mwenzake James Mahangi.

Kwa Kanda hiyo ya Nyasa wagombea walikuwa watatu na mmoja akiwamo Daniel Mwambipile, ambaye amekatwa.

Kanda ya Magharibi, wagombea wote wanne wameteuliwa ambao ni Dickson Matata, Gaston Garubindi, Mussa Mafure Na Ngassa Mboje.

 Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, Kanuni ya 7.5 ya CHADEMA yenye vipengele 13 inaeleza sifa ambazo kila mgombea kulingana na nafasi yake anatakiwa kuwa nazo na ndiyo iliyotumika kuteua wagombea hao.

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, Mrema alisema watia nia watakaokatwa itabidi wakubali matokeo kwa kuwa, zipo kazi nyingine za chama chao wataendelea kufanya.

“Maana ya usaili ni kwamba, tuna vigezo vyetu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni yetu, ni sifa gani viongozi wa ngazi gani wanapaswa kuwa nayo.

“Kwa hiyo ndiyo maana kama mtu akikutwa hana hizo sifa, basi moja kwa moja anaweza akaenguliwa, akashauriwa atumikie majukumu mengine kwa sababu bado ni chama kimoja, nafasi ni chache, wanachama wote hawawezi kuwa viongozi,” alisema.

Kwa mujibu wa Mrema, uchaguzi kwenye kanda hizo unatarajiwa kufanyika Mei 29, mwaka huu.

Kuhusu mambo mengine yaliyojiri kwenye kikao cha kamati kuu, anayesubiriwa ni Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, kuweka wazi wakati wowote.