Mtanzania ateuliwa ujumbe bodi ya GEF

By Restuta James , Nipashe
Published at 06:33 PM Apr 17 2024
Bernice Fernandes.
PICHA: MAKTABA
Bernice Fernandes.

MTANZANIA Bernice Fernandes, ameteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Jumuiya ya Tamasha la Kimataifa la Ujasiriamali (GEF), ambayo pamoja na mambo mengine itaandaa tamasha la mwaka huu ambalo mmoja wa wazungumzaji anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama.

Bernice ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa kampuni ya Accelerate Business Group inayojishughulisha kutoa ushauri, usimamizi na uongozi wa biashara.

Anatajwa kuwa kiongozi mahiri wa masuala ya ujasiriamali mwenye uwezo wa kutoa maarifa muhimu na mwongozo wa kimkakati kwa biashara.

Kitaaluma Benice ana shahada ya uzamili katika ujasiriamali, katika biashara ya kimataifa na shahada ya kwanza katika masuala ya fedha na kuteuliwa kwake kama mwakilishi pekee wa Tanzania katika bodi hiyo ya Kimataifa, kunamwongezea chachu ya kukuza ujasiriamali na kuendeleza uongozi wa wanawake nchini.

Akizungumza na Nipashe Digital leo Aprili 17, 2024 jijini Dar es Salaam, Benice amesema ni heshima kwake na nchi na kwamba atatumia nafasi hiyo ya kimataifa kuitangaza Tanzania kwenye dunia ya biashara.

Amesema kuteuliwa kwake kutampa uzoefu wa kukuza ujasiriamali na kuleta mabadiliko chanya katika kiwango cha kimataifa, akiwa na shauku ya uvumbuzi na uwezeshaji.

"Nina heshima kujiunga na bodi kubwa ya Tamasha la Kimataifa la Ujasiriamali…ninatazamia kushirikiana na wajumbe wenzangu wa bodi na washirika wetu ili kuleta manufaa na mabadiliko kwa wajasiriamali duniani kote."

Tamasha la Kimataifa la Ujasiriamali ndilo tukio kubwa zaidi linalokutanisha watu wa kada mbalimbali kutoka pande zote za dunia wakiwamo viongozi wakuu wa nchi, watunga sera, mashirika ya kimataifa, wavumbuzi na wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Bodi hiyo ina jumla ya wajumbe 21 kutoka nchi mbalimbali akiwamo Summy Francis, ambaye ni rais wa Wajasiriamali Vijana Afrika.

Tamasha la mwaka huu imepangwa kufanyika katika Kijiji cha Ujasiriamali kilichopo jimbo la Ondo nchini Nigeria, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Ujasiriamali Duniani kuanzia Novemba 11 hadi 13, 2024.

Mbali ya Obama, baadhi ya wazungumzaji wengine kwenye tamasha hilo ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la biashara duniani (WTO), Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na mwanamuziki wa Marekani mwenye asili ya Senegali, Aliaune Akon.