Mwanga mpya

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:08 AM Jun 19 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Kamati Maalum ya Kutathmini Hali ya Utendaji na Uchumi wa Vyombo vya Habari Tanzania Bara kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mwandishi Mbobevu Tido Mhando wakati wa Kongamano hilo.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Kamati Maalum ya Kutathmini Hali ya Utendaji na Uchumi wa Vyombo vya Habari Tanzania Bara kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mwandishi Mbobevu Tido Mhando wakati wa Kongamano hilo.

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa miezi sita kwa wizara na taasisi za umma zinazodaiwa na vyombo vya habari kuhakiki madeni na kukaa pamoja kujadili watakavyoyalipa.

Amewakumbusha waandishi kuandika habari zenye kuleta mawazo kinzani ya kuijenga nchi badala ya kuchochea migogoro na mipasuko ya kutishia amani ya nchi.

Pia, aliwapongeza waandishi mbalimbali waliopata tuzo za kimataifa kwa kuiwaikilisha Tanzania na kuiletea sifa, akiwamo Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Beatrice Bandawe, aliyetunukiwa tuzo ya mwanamke kiongozi kwenye chumba cha habari Afrika, inayotolewa na Umoja wa Wachapishaji Duniani (WAN IFRA) akiwa ni Mtanzania wa kwanza.

Wengine ni Mhariri Mtendaji gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, aliyechaguliwa kuwa Rais wa Jumuiya ya Wahariri Mashariki mwa Afrika, Ernest Sungura, Mwenyekiti wa kwanza Mtandao wa Mabaraza Huru barani Afrika na Kajubi Mukajanga kuwa kiongozi wa Baraza la Vyombo vya Habari Afrika Mashariki.

Rais Samia aliyasema hayo jana wakati akihutubia Kongamano la pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia madeni ya vyombo vya habari, aliahidi serikali itayalipa ifikapo Desemba, mwaka huu.

Alisema ataiagiza Wizara ya Fedha kufanya uhakiki wa madeni ya serikali ili yanayolipika yalipwe huku akiahidi kusimamia suala hilo.

Aliwakumbusha wamiliki wa vyombo vya habari wakati serikali inawalipa madeni hayo, wawalipe wafanyakazi wao mishahara yao. Alisema kutowalipa kunapunguza ari ya kufanya kazi na kudhorotosha maendeleo ya sekta ya habari.

Aliwashangaa waandishi wa habari kuwa hodari kuandika mambo ya watu wengine wakati wao wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kutolipwa mishahara na waajiri wao na hawasemi chochote.

Kadhalika, alisema sasa ni wakati wa vyombo vya habari kujiendesha kibiashara ili kuepuka madeni yasiyolipika yanaonekana kuwa mengi na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuwatia hasara.

Akizungumzia mabadiliko ya teknolojia, alisisitiza umuhimu wa kufikiria kuwekeza kwenye habari za mtandaoni kwa kuwa wasomaji wa magazeti ya kuchapisha wamepungua na pia malighafi za kuchapishia zimepungua kutokana na wazalishaji wakuu ambao ni nchi ya Ukraine kuathirika na vita, hali inayochangia kudorora kwa biashara zao.

UWAJIBIKAJI 

Rais Samia alisema, amefanya juhudi kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na kusisitiza ni wajibu wao kuutumia kwa weledi na kuzingatia dhana ya uwajibikaji kwa sababu vina kazi muhimu ya kuunganisha serikali na wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani, alisema kalamu za waandishi wa habari zinahitajika kwa ajili ya kujenga na si kubomoa kwa kuleta migongano ya kisiasa.

"Kwa maneno mengine msitoboe dau tunalosafiria, ndani ya hilo dau tupo wote, ukitoboa yakiingia maji tunazama wote, msiingie kwenye mtego wa kurarua nyuzi zinazounganisha kitambaa cha taifa letu," alisema. 

Alisema uhuru wa vyombo vya habari haumaanishi kutoa lugha ya matusi, kashfa wala kejeli bali kutoa mawazo kinzani yenye lengo la kuboresha na kuijenga nchi ili kuleta maendeleo.

Alivitaka vyombo hivyo kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia huku vikijua wajibu wao wa kulinda mila, desturi na utamaduni na usalama wa kisiasa wa taifa hilo na si kuyahamasisha kwa kisingizio cha biashara.

Aliwakumbusha kutumia kalamu zao kuandika mambo yanayojenga nchi kwa kuwa yakiandikwa mambo mabaya yakasomwa nje ya nchi sifa ya nchi nzima inaharibika na si ya mtu mmoja.

Alisema kongamano hilo litumike kujitathmini ni wapi wanafanya vyema na wapi hawafanyi vizuri na kupanga mikakati ya namna ya kujiboresha kwa manufaa ya vyombo vyao na nchi kwa ujumla.

ASISITIZA UCHAMBUZI 

Amesisitiza vyombo vya habari kufanya uchambuzi wa kina taarifa wanazozipokea kabla ya kuziandika kwa kuwa nyingi zimekuwa zikiandikwa kama zilivyo na wakati mwingine kuleta taharuki.

Aidha, kuandika habari zinazokubalika na jamii badala ya kupata umaarufu na matokeo yake kuharibu hadhi ya mwandishi na chombo cha habari. 

Alisema kuna baadhi ya waandishi wanachukua habari zilizoandikwa na mataifa mengine kuhusu nchi hiyo na kuziandika kama zilivyo bila ya kuzifanyia uchambuzi na kuwasihi kuwa wafafanuzi wa hoja kwa ajili ya kulinda hadhi zao wenyewe na nchi yao.

HATUSHINDANI 

Alisema vyombo vya habari si mshindani wa serikali bali ni mdau na mshiriki muhimu wa shughuli za serikali na kuuhabarisha umma masuala ya nchi yanayochochea maendeleo.

"Huko nyuma kipindi fulani vyombo vya habari na serikali vilikuwa vinavutana, wao wamevuta na sisi tumevuta, lakini tuliona hatutofika pahali pazuri hivyo tuliamua kukaa sehemu moja, kuzungumza na kufanya kazi kwa pamoja," alisema. 

Alisema serikali haina budi kuweka mifumo ya kisera, kisheria na taasisi inayolenga kuimarisha uhuru wa mazingira kwa waandishi wa habari. 

Alivishukuru vyombo hivyo kwa jinsi vinavyoshirikiana na serikali kutoa habari kwa umma kuhusu mambo yanayoendelea kwenye jamii ikiwamo harakati za maendeleo na hata majanga kama vile maporomoko ya Hanang' na athari za mvua za El-nino zilitokea miezi michache iliyopita.

HABARI ZA VIJIJINI 

Alisisitiza habari za vijijini ziripotiwe na vyombo vya habari vya jamii, wananchi wa maeneo hayo wapate kuzisikia, kwa kuwa taarifa nyingi zinaandikwa na vyombo vya kitaifa kama vile ITV, TBC, UTV.

Aliwaagiza wadau wa habari kuipelekea serikali mapendekezo ya kuundwa kwa mkakati wa mawasiliano nchini ili kuboresha sekta hiyo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema maboresho makubwa aliyoyafanya Rais Samia yameipandisha nchi chati kimataifa katika kuimarisha uhuru wa habari.

Alisema hilo limethibitishwa na Ripoti ya World Press Freedom Index ya mwaka 2024 inayoonyesha kuwa Tanzania imeongoza kwa nchi za Afrika Mashariki na duniani kushika nafasi ya 97 kutoka 143. 

Alisema pia sifa hiyo imechochewa pia na mabadiliko ya mtanzamo wa waandishi wa habari kutokana na uzalendo mkubwa baina yao kwa kuwa katika utoaji taarifa zinazohusu nchi hiyo wametanguliza maslahi ya nchi.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, alisema wizara hiyo imekamilisha Sera ya Habari na wanatarajia kuizindua.

Alimshuruku Waziri Nape kwa kuwasaidia kuwapa wataalamu wengi ili kuhakikisha sheria hiyo inakuwa na maudhui sawa na Sheria ya Habari ya Tanzania Bara kwa kuwa wote wanatoka katika nchi moja.

Mwenyekiti wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRi), Ernest Sungura aliiomba serikali kuondoa ukomo wa uwekezaji wasiokuwa wa Tanzania kumiliki hisa na kuwaruhusu wamiliki zaidi ya asilimia 49 ili kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.

Alitaja changamoto zinazowakabili waandishi wa habari kuwa ni kufanya kazi bila mikataba na takwimu zikionyesha kuwa ni asilimia 80 wanaishi katika hali hiyo tofauti na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. 

Aidha, aliiomba serikali kupanua uhuru wa vyombo vya habari nchini ili kumpa uhuru kila mwandishi wa kutoa maudhui huku wakiimarisha misingi kusimamia maadili ya weledi katika kazi.

Akisoma Taarifa ya Hali ya Waandishi wa Habari, Utendaji na Uchumi wa Vyombo vya  Habari nchini, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Tido Muhando, aliainisha mambo waliyoyaona kuwa ni changamoto katika vyombo vya habari ikiwamo kuidai serikali na sekta binafsi madeni makubwa na ya muda mrefu.

Alisema hali hiyo imesababisha vyombo hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati ikiwamo kuwalipa wafanyakazi mishahara na kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Aidha, alisema kutokana na hofu ya usalama wao, waandishi wa habari wameacha kuandika maudhui yanayolenga uwajibikaji na kudhoofisha waandishi kuzingatia uwajibikaji wa umma na kuwa na kizazi kisichofikiria sawa sawa, wengi wamebobea kwenye habari za burudani, vichekesho.

Kamati hiyo ilipendekeza pamoja na mambo mengine kuboreshwa kwa sera ya habari ili kuruhusu wawekezaji wa nje kumiliki hisa kwa asilimia 75, kwa sasa sera hiyo inaonyesha wawekezaji hao wanaweza kuwekeza chini ya asilimia 50.

Ilipendekeza kuwapo na mfuko wa mafunzo kwa vyombo vya habari yatakayowezesha kuletwa kwa kampuni za nje za teknolojia kwa ajili ya mafunzo pamoja akili bandia itumike katika vyombo vya habari.