Mwenyekiti Samia aibuka na vikwazo vinne Afrika

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 03:22 PM May 15 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika, jijini Paris, Ufaransa.

RAIS Samia Suluhu Hassan ametaja mambo manne yanayokwamisha juhudi za upatikanaji wa nishati safi ya kupikia Afrika, ambayo yanatakiwa kutatuliwa ili kufikia lengo la dunia la kuondoa hewa ukaa.

Samia ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa kwanza wa nishati safi ya kupikia jijini Paris, Ufaransa, uliowakutanisha takribani wawakilishi 1,000 kutoka karibu nchi 50.

Mkutano huo unafanyika wakati matumizi ya nishati isiyo salama katika kupikia yakishika kasi. 

Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati wa Kimataifa (IEA), watu bilioni 2.3 kutoka nchi 128 duniani wanavuta hewa chafu kwa kutumia njia isiyo salama kupikia, ikiwamo mkaa.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine, utajadili namna ya kusaidia mabilioni ya watu kubadilisha mfumo wa kupika ambao unazalisha hewa hatari kwa afya na kupunguza vifo zaidi ya milioni vinavyotokea kabla ya wakati, vingi vikiwa katika bara la Afrika.

Amesema kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa nishati safi na endelevu ya kupikia  kwa bei nafuu, kaya nyingi  hususan vijijini, zinapata ugumu wa kuitumia. Alitaja sababu kubwa kuwa ni gharama kubwa, upatikanaji mdogo na minyororo duni ya ugavi.

Rais Samia ametaja sababu nyingine kuwa ni ufadhili hafifu na ukosefu wa uelewa kuhusu fursa za kiuchumi katika suala hilo, huku maendeleo ya  upatikaji wa suluhisho yakiwa yamezuiwa na ukosefu wa utafiti na ubunifu wa kutosha. 

Sababu ya tatu, kwa mujibu wa Samia, ni ukosefu wa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wote. 

Amesema kikwazo kingine kipo kwenye kuzipatia suluhisho changamoto hizo, akieleza kuwa msisitizo lazima uwekwe kwenye kutambua suluhisho linalowezekana na nafuu.

Amesema Afrika yenye kiwango cha juu zaidi cha ongezeko la watu na rasilimali zote muhimu, linashika nafasi ya chini katika upatikanaji wa nishati safi ya kupikia hali inayowaweka watu wake katika hatari kiafya. 

“Zaidi ya Waafrika milioni 900 wanategemea masuluhisho yasiyo safi ya nishati ya kupikia ambayo huchangia katika uharibifu wa mazingira, kupoteza baianowai na hatari za kiafya,” amesema. 

Kwa mujibu wa IEA, kutumia nishati safi wakati wa kupikia kama vile gesi au umeme kutaokoa uzalishwaji wa tani 1.5 za hewa chafu ifikapo mwaka 2030. 

Amesema kwa kuzitambua changamoto  hizo, Tanzania hivi karibuni ilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10 wenye lengo la kuhakikisha  asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati mbadala ya kupikia kufikia mwaka 2034.

Pia amesema mkakati huo unadhamiria kuanzisha mfuko wa kitaifa ili kusaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na Waziri Mkuu atausimamia kwa hali ya juu ili kulinda afya za watumiaji na kuokoa mazingira.

“Kutokana na mzigo mkubwa wanaobeba wanawake, Tanzania itaendelea kutetea Programu ya Msaada wa Kupika kwa Nishati Safi ya Afrika sio tu kushughulikia athari za mazingira na afya bali kuwawezesha wanawake kama mawakala wa mabadiliko ndani ya jamii zao,” amesema.

Samia amesema kutumia nishati safi kupikia, kunaondoa athari chanya kwa watumiaji katika nchi zao, dunia na mazingira kwa jumla  hivyo basi ni muhimu ajenda hiyo kuwa kipaumbele kwa Afrika. 

Amelipongeza IEA kwa kutangaza mwaka 2024 kuwa mwaka wa kupika kwa nishati safi na kwa kuitisha mkutano huo, na wote waliohudhuria na kujadili ili kuhakikisha  nishati safi kwa wote inapatikana.

Kwa mujibu wa Rais Samia, ajenda ya nishati safi ya kupikia barani Afrika ikipewa msukumo itasaidia kutunza mazingira kwa kuongeza maendeleo ya vijana na kuwapa wanawake fursa zaidi ya kushiriki shughuli zingine za maendeleo na uzalishaji na hivyo kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa.

Amesema ili kufikia ajenda hiyo kunahitajika mifumo ya msaada na sera zinazotoa mwongozo wa  kupatikana kwa nishati hiyo kwa bei nafuu na teknolojia kote barani.

Amesema ili kufikia lengo la kifedha ambalo IEA imekadiria ili kupatikana  nishati safi kwa wote ifikapo mwaka 2030 mkutano huo unapaswa kuelekeza maombi ya ufadhili kwa wadau kama vile  Mfuko wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Støre, amesema maboresho ya nishati ya kupikia yatapunguza uzalishwaji wa hewa chafu, kuboresha afya na  kuunda fursa za ukuaji wa kiuchumi. 

“Norway ni mfuasi thabiti wa kupika kwa nishati safi, na nimefurahi kutangaza leo kwamba tumejitolea kuwekeza takriban dola milioni 50 katika sababu hii muhimu," amesema. 

Mkurugenzi Mtendaji wa IEA, Fatih Birol, amesema dola bilioni 2.2 zilizopatikana katika mkutano huo ni mwanzo nzuri wa safari ya kutokomeza matumizi nishati isiyosalama kupikia na kusaidia upatikanaji wa haki za msingi kama vile afya bora, usawa wa kijinsia na elimu.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinwumi Adesina, amesema kwa kushirikiana na nchi mbalimbali wameongeza  ufadhili katika kusukuma ajenda ya nishati safi  kupikia hadi dola milioni 200 kila mwaka kwa muongo mmoja ujao, kupitia Mfuko wa Nishati Endelevu kwa Afrika (SEFA).