Mwili wa mwenye ualbino wakutwa bila viungo, Rais Samia aingilia kati

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:21 AM Jun 19 2024
Rais Samia Suluhu Hassan katika picha ya kuunganisha na mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) aliyetekwa na kuuawa kwa kukatwa viungo vya mwili wake.
Picha: Nipashe Digital
Rais Samia Suluhu Hassan katika picha ya kuunganisha na mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) aliyetekwa na kuuawa kwa kukatwa viungo vya mwili wake.

VILIO vimetawala wakati mwili wa mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) ukiopolewa baada ya kukutwa kwenye karavati, huku baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa.

Mtoto huyo alichukuliwa mikononi mwa mama yake Mei 20, mwaka huu na watu wasiojulikana. Mwili wake umegundulika baada ya siku 19. 

Juzi wananchi walishuhudia mwili wa mtoto huyo ukiopolewa ukiwa umefungwa katika mfuko wa sandarusi, huku Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Yusuph Daniel, akithibitisha jeshi hilo kuwashikilia wanaume wanne kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo la kikatili.

Kutokana na tukio hilo, Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimeomba kuteta na uongozi wa juu serikalini, kikihofia usalama wa kundi hilo katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Mei 20, mwaka huu, mtoto huyo, mkazi wa Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, wilayani Muleba, mkoani Kagera, alichukuliwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba, Benjamin Mwikasyege, akizungumza na waandishi wa habari akiwa eneo ulikopatikana mwili huo, alisema ulikutwa chini ya daraja, ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi, huku baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa.

"Mwili umekutwa chini ya daraja (lililoko barabara ya Makongora, Kitongoji cha Kabyonda, Kijiji cha Balele, Kata ya Ruhanga) kwenye karavati ukiwa umefungwa kwenye mfuko wa sandarusi. Kuna maji kidogo na kuna mfereji. 

"Sote tunalaani tukio hili hasa kumpoteza mtoto huyu mwenye ualbino, kuna baadhi ya viungo ambavyo vimetolewa. Mwili huo umewekwa na watu ambao hawajafahamika. Baada ya kuufungua, viongozi wameendelea kuukagua," alisema Mwikasyege.

Alisema kuwa kupitia Jeshi la Polisi wataendelea na taratibu zao za kiuchunguzi, akisisitiza kuwa wote waliohusika, watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Kuua kwa kukusudia si tu kwamba ni kosa la jinai lenye adhabu ya hukumu ya kifo mahakamani, bali pia ni ukiukwaji wa Katiba ya Nchi, Ibara ya 14 inayoelekeza "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria."

Katibu Tawala Mwikasyege aliomba wakazi wa Muleba, Kamachumu na Ruhanga watoe ushirikiano kwa serikali ili kazi ya polisi iwe rahisi.

"Tunajua tutawapata kwa namna ambavyo serikali imejipanga, lakini tunahitaji ushirikiano wa wananchi wa Ruhanga ambako mwili huu tumeupata. Baada ya hapa kama serikali tutahusika kuhakikisha mwili unahifadhiwa vizuri.

"Tutaukabidhi kwa familia, lakini tutahusika kwa asilimia 100 mtoto huyo tunamhifadhi vizuri katika nyumba yake ya milele, tutakapotoa ratiba ya lini na wapi, wote tujitokeze ikiwa ni ishara ya kulaani kile kilichofanyika kuwa kila mmoja wetu hakubaliani nacho," alisema Mwikasyege.

KAULI YA TAS

Kaimu Katibu Mkuu wa TAS, Abdillah Omary, akizungumzia tukio hilo jana, alisema matarajio yao yalikuwa kumpata mtoto huyo akiwa hai, lakini kilichotokea kimewashtua.

Alisema wanahitaji kuonana na mamlaka kubwa ndani ya nchi ili kusaidia usalama wa kundi hilo, ikizingatiwa mwaka huu kuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani. Kumekuwa na matukio ya ukatili dhidi ya kundi hilo wakati wa mchakato wa uchaguzi nchini.

"Kama mwenye ualbino na mzazi mwenye watoto, ninajaribu kuwaza kwa siku zote ambazo mtoto huyo alichukuliwa mikononi mwa mama yake, alikuwa katika hali gani, wakati anafanyiwa madhira hayo yote alipitia hatua gani za uchungu," alisema.

Omary alikumbusha jamii kwamba ualbino hauwezi kufutwa nchini. Wanaodhani kundi hilo litawapa utajiri waondokane na fikra hizo na kila mmoja awe na wajibu kuhakikisha ulinzi na usalama kwao.

Alisema kuwa mwaka 2023, matukio yaliyojitokeza yalihusu ufukuaji makaburi na vitisho kwa kundi hilo na kwa mwaka huu, tayari kuna matukio mawili, likiwamo la kijana kujeruhiwa na wasiojulikana wakati akicheza nyumbani kwao.

Jana bungeni, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Khadija Taya, maarufu Keysha, aliomba mwongozo wa Spika, akitaka lijadili usalama wa wenye ualbino wakati wa mchakato wa uchaguzi. 

Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alisema mbunge huyo alikosea kanuni wakati wa kuwasilisha hoja yake na kumwelekeza kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ili amweleze vizuri kuhusu suala hilo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Yusuph Daniel, aliiambia Nipashe jana kuwa hadi sasa wanashikilia wanaume wanne kutokana na tukio la Mei 20 mwaka huu, mwili wa mtoto huyo unasubiri ndugu zake ili taratibu za maziko zifanyike. Gharama zinabebwa na serikali.

Rais Samia Suluhu Hassan alisema jana kuwa kifo hicho cha mtoto mdogo mwenye ualbino kimemgusa, akitaka washiriki wa Kongamano la Sekta ya Habari kusimama kwa muda na kuomba kwa ajili ya kundi hilo.

RAS AFA AJALINI

Mkoani Kilimanjaro, ajali ya barabarani imekatisha uhai wa Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dk. Tixon Nzunda, aliyekuwa akiwahi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kumpokea  Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango na ujumbe wake.

Dk. Nzunda na dereva wake walipoteza maisha jana alasiri baada ya gari lake aina ya VXR kugongana uso kwa uso na lori la kubeba nishati ya gesi safi, mali ya Kampuni ya Orange Gas, lenye namba za usajili T 655 ABY, aina ya Scania lililokuwa likitokea Arusha kwenda Moshi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, akitangaza kifo cha Dk. Nzunda, akisema Katibu Tawala huyo na dereva wake walipoteza maisha saa 8:30 mchana katika eneo la Mjohoroni (Palestina), wilayani Hai.

*Imeandaliwa na Romana Mallya na Godfrey Mushi.