Mwili wa RAS Kilimanjaro waagwa, Waziri Ummy aeleza upekee wake

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 09:55 AM Jun 21 2024
Mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro Dk. Tixon Nzunda ukifikishwa nyumbani kwake katika eneo la Shanty Town katika manispaa ya Moshi.
Picha: Mtandao
Mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro Dk. Tixon Nzunda ukifikishwa nyumbani kwake katika eneo la Shanty Town katika manispaa ya Moshi.

WAZIRI wa afya, Ummy Mwalimu, amesema wema na uadilifu wa aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Tixon Nzunda kwa Watanzania na taifa lake, unamfanya ashindwe kumwelezea alikuwa mtu wa aina gani.

Akizungumza jana katika Mji wa Moshi, wakati wa ibada ya kuuaga mwili wa Dk.Nzunda, Waziri Ummy alisema kiongozi huyo ameacha pengo kubwa kwa nchi.

Dk. Nzunda (56) na dereva wake, Alphonce Edson (54), walipoteza maisha kwa ajali ya gari Juni 18 mwaka huu saa 8:30 mchana katika eneo la Mjohoroni (Palestina), Kata ya KIA, Wilaya ya Hai, baada ya gari lake aina ya Toyota Landcruiser GXR, lenye namba STM 7476, kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 655 ABY, mali ya Kampuni ya Orange Gas.

Walikuwa wanakwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kumpokea Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango aliyekuwa anakwenda mkoani Arusha.

Waziri Ummy alisema, "Nimeshindwa kuelezea wema wake kwangu na kwa taifa la Tanzania katika nyadhifa mbalimbali alizoshika hasa kwa kuhudumia wananchi wa Tanzania." 

Mwili wa Dk. Nzunda ulisafirishwa jana jioni kutoka Kilimanjaro kwenda nyumbani kwake Goba, wilayani Ubungo, Dar es Salaam kabla ya kwenda kuzikwa kijijini kwao Mpemba-Momba, wilayani Mbozi, mkoani Songwe Juni 22. 

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema kifo cha Dk. Nzunda ni pengo lisilozibika kwa sasa na ni ngumu kusema chochote na hajui ataanzia wapi kutokana na utendaji, ushauri na uwajibikaji wake katika mkoa huo.

"Sijui mafaili nitayapeleka wapi, maana wakati wote tulikuwa tuna ushirikiano mkubwa sana. Tunasaidiana kama ndugu na siyo viongozi, Nilikuwa nikimwomba ushauri, alikuwa akinitia moyo na hakukuwa na gumu lililoshindikana kwake, hakika sijui nitaanzia wapi.

"Sijaanza kufanya naye kazi Mkoa wa Kilimanjaro, bali maeneo mbalimbali hasa nikiwa Manyara. Sisi tulikuwa zaidi ya ndugu, tunafanya kazi kwa umoja na ushirikiano.

"Taarifa za kifo chake nilizipokea kwa masikitiko makubwa sana, sikukuu ya Eid el-Adha tulikuwa pamoja, yeye na watoto wake.

"Ninashindwa kuelezea nini niseme. Tulikuta mkoa umeyumba, ila tulishaanza kuunyosha ikiwa ni pamoja na kumaliza urasimu wote," alisema Babu.

Aliitaka familia kuhakikisha inaishi yale aliyoyaishi Dk. Nzunda na kuleta mabadiliko kwenye jamii kama ilivyokuwa adhima yake.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafue, alisema Dk. Nzunda atakumbukwa kwa kuwa mtu wa haki na kusogeza maendeleo ya mkoa, kutokomeza urasimu na kutafuta majibu ya kila tatizo.

"Familia, Mungu awatie nguvu maana mlikuwa na baba wa mfano, alitokomeza urasimu, alisukuma maendeleo, alikuwa mwadilifu na makini kwenye kazi, hivyo tunaomba tuige na kuleta mabadiliko," alisema Saashisha.

Akitoa salamu, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa, alisema: "Tulipokea kwa masikitiko sana msiba huu, alikuwa ni mtu wa ushirikiano, upendo na mwelekezaji wa kila mara. Tuliweka mipango mingi. Hakika tumepoteza kiungo muhimu kwa makatibu tawala nchi nzima.

"Tumefanya naye kazi nyingi tu, alikuwa mshauri mwema, hakuwahi kunyanyua mabega licha kuwa na vipaji vingi. Alikuwa na misimamo isiyoyumbishwa. Alikuwa anapenda watu, siyo mchoyo."