NACTVET yatangaza Udahili mwaka wa masomo 2024/25

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:16 PM May 28 2024
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Adolf Rutayuga.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Adolf Rutayuga.

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetangaza kufungua dirisha la Udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada katika kozi zote zinazosimamiwa na NACTVET kuanzania Mei 27 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Maonesho ya Ubunifu na Ujuzi yanayoendelea Mjini Tanga Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Adolf Rutayuga amesema dirisha hilo limefunguliwa rasmi Mei 27 mwaka huu ikiwa ni fursa katika Maonesho hayo wakaanza kuomba kutokana na uwepo ushiriki wa Vyuo vyote katika Maonesho.

Dk.Rutayuga amesema kuwa maombi ya udahili kwa kozi ambazo si za Afya na Sayansi Shirikishi na kozi za Afya na Sayansi Shirikishi zitolewazo katika Vyuo Vya Zanzibar yatumwe moja kwa moja kwenye Vyuo husika kuanzia Mei 27 hadi Julai 14 mwaka huu kwa awamu ya kwanza.

Hata hivyo amesema maombi ya kozi za Afya na Sayansi Shirikishi kwa upande wa Tanzania Bara yatafanyika kupitia mfumo wa udahili wa pamoja (CAS) unaopatikana katika tovuti ya Baraza www.nactvet.go.tz kuanzia Mei 27 hadi Juni 30 mwaka huu kwa awamu ya kwanza.

Aidha Dk.Rutayuga amesema kuwa zinazoombwa na vyuo vinavyotoa kozi hizo vimeorodheshwa kwenye Kitabu cha Muongozo wa Udahili kwa mwaka wa masomo 2024/2025 ambao muongozo huo unapatikana kwenye tovuti ya www.nactvet.go.tz.

Dk.Rutayuga amewataka waombaji wote kuandika taarifa zao kwa usahihi na umakini pamoja na kutunza kumbukumbu watazopatiwa na Baraza bila kumpatia mtu mwingine yeyote ili kuepusha usumbufu katika zoezi zima la maombi ya kujiunga na kozi kwenye vyuo mbalimbali.