Naibu Spika: Zanzibar ina uhaba wataalamu afya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:40 AM May 20 2024
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma.
Picha: Maktaba
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma.

NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, amesema Zanzibar inamahitaji makubwa ya wataalamu wa sekta ya afya.

Naibu Spika: Zanzibar ina uhaba wataalamu afya Hivyo, ameiomba Global Education Link (GEL) kuwaunganisha wanafunzi wa visiwa hivyo na vyuo vikuu nje ya nchi, ili iweze kupata wataalamu wa kutosha.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na ujumbe wa Global Education Link ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Abdulmalik Mollel, uliotembelea Baraza la Wawakilishi kwa mwaliko wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdulgulam Hussein.

Amesema maendeleo ya nchi yanahitaji vijana wenye ujuzi mbalimbali, hivyo mchango wa taasisi hiyo kwenye sekta ya elimu ni wa kuigwa.

“Nawapongeza mnafanyakazi kubwa na ngumu inayohitaji uvumilivu sana. Mimi nilishawahi kusema kwenye Baraza la Wawakilishi kuhusu wanafunzi kukosa nafasi za kazi wanazotaka hapa visiwani kwa hiyo kama kuna fursa ya kuwapeleka nje ya nchi ni jambo jema sana,” amesema. 

Amesema amefurahi kusikia Global imekuwa ikifanya kazi ya kuwabadili mitazamo vijana wa kitanzania na kuwajenga kwa ajili ya kujiajiri zaidi badala ya kuhangaika kutafuta ajira kila wanapohitimu masomo yao.

“Lazima tuwajenge vijana waweze kujitegemea, tumejisahau kidogo kwenye malezi vijana wengi hawawezi kazi kwa hiyo kuna haja ya kuwabadili fikra zao ili waweze kujitegemea na hata wakipata kazi wafanye kazi kwa bidii,” amesema.

Amesema Zanzibar kuna vijana wengi wanaohitaji kupata ufadhili wa elimu ya juu, lakini wanakwama kwa kukosa maarifa ya sehemu wanayoweza kupata msaada, hivyo aliiomba Global iwe kiunganishi baina ya vijana hao na taasisi mbalimbali.