Nchimbi atia neno kuwambuka mashujaa vita ya Majimaji

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:08 PM Apr 22 2024
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi.
PICHA: HALFANI CHUSI
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amewataka watanzania na Serikali kuendelea kuenzi na kuwakumbuka mashujaa waliokufa wakati wa vita ya Majimaji.

Nchimbi ameyasema hayo leo Songea alipotembelea Makumbusho ya vita hiyo mjini Songea, ambapo pia alipata nafasi ya kutembelea makaburi ya mashujaa 67 wa vita hiyo, ambao kati yao; 66 walinyongwa na Wajerumani, huku mmoja akipigwa risasi. Vita hiyo ilipiganwa kuanzia mwaka 1905-1907.

"Mashujaa waliozikwa hapa walikataa kutawaliwa waliona bora kufa kuliko kutawaliwa na wageni kutoka nje ya nchi. Tutaendelea kuenzi na kuthamini utamaduni wa Mtanzania" amesema Nchimbi Katika viunga vya makaburi hayo.

Akiwa Katika mkutano wa hadhara na wafuasi wa chama hicho baadaye baada ya kutembelea makumbusho hayo aliwataka mabalozi wa chama hicho kuwekeza nguvu katika kuimarisha chama.

"Unapokwisha uchaguzi nongwa za uchaguzi hatuzitaki, unakuta uchaguzi umeisha miaka minne imepita, wewe bado unanongwa mpaka leo; aliyeshindwa ananongwa na aliyeshindwa ananongwa hii sio sawa, itakigawa chama,” amesema na kuongeza;

"Sio lazima kila mtu akuunge mkono wewe nani, ukiisha uchaguzi ungana na wote uliogombea nao shirikianeni mjenge chama."

Vilevile Balozi Nchimbi, amewataka wafuasi wa chama hicho kuchagua viongozi wanaotokana na CCM, huku akisisitiza kuwa hakuna viongozi wa kuipeleka nchi mbali, nje ya viongozi wanaotokana na chama hicho.

Awali Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo wa chama hivyo, Amosi Makalla amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia hali ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho, uhai wa chama, maandalizi ya uchaguzi, na utatuzi wa kero za wananchi.