WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema nyama ya mbuzi inaongoza katika mauzo nje ya nchi na inachangia asilimia 70.1 ya mauzo yote.
Amebainisha hayo kwenye makabidhiano ya Kituo Atamizi cha Vijana cha ufugaji mbuzi kibiashara kilichojengwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kwa ufadhili wa Serikali ya Denmark kupitia Mfuko Binafsi wa Kusaidia Wakulima (PASS TRUST).
Amesema mauzo ya nyama nje ya nchi yameendelea kuongezeka hadi kufikia Aprili, 2024 tani 11,682.3 (zikiwamo tani 870.7 za nyama ya ngómbe, tani 8,059.38 za nyama ya mbuzi, tani 2,715.5 za nyama ya kondoo, tani 27.5 za nyama ya kuku na tani 9.3 za nyama ya nguruwe) zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 50.3 zilikuwa zimeuzwa nje ya nchi.
Amesema nyama ya mbuzi imeendelea kuongoza katika mauzo hayo na kwamba serikali inaendelea na jitihada za makusudi ili kuboresha utendaji wa sekta hiyo, ikilenga kuvutia na kunufaika zaidi na masoko ya kimataifa.
Amebainisha kuwa kwa sasa kuna nchi 12 zinazonunua nyama kutoka Tanzania na mikakati ni kuweka miundombinu na sera rafiki zaidi ili kuboresha sekta hiyo.
Majaliwa amesema serikali imeamua kuongeza Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Sh. bilioni 66 hadi Sh. bilioni 295.9 mwaka huu ili kusukuma mbele mabadiliko makubwa na maendeleo katika sekta hiyo.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara na wasindikaji wa nyama kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi kushirikiana na kituo hicho, ili kupunguza tatizo la upatikanaji ya mifugo bora kwa ajili ya uzalishaji wa nyama na mazao yake.
Majaliwa amesema: “Nazisihi taasisi za fedha zione fursa hii ili kukaa na wadau katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji na usindikaji wa nyama ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji, nitoe wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ina jukumu la kusimamia sekta ya mifugo, iendelee kuweka mazingira bora ya uwekezaji ili kuwezesha sekta binafsi kufanya uwekezaji wenye tija na faida”.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED