Polisi Shinyanga yakamata mali za wizi, dawa za kulevya

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 03:47 PM Apr 17 2024
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Kennedy Mgani akionyesha vifaavya wizi walivyovikamata.
PICHA: MARCO MADUHU
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Kennedy Mgani akionyesha vifaavya wizi walivyovikamata.

OPERESHENI ya wiki tatu iliyofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, imezaa matunda baada ya jeshi hilo kufanikiwa kukamata watuhumiwa wa matukio ya uharifu, mali zinazosadikiwa kuwa za wizi pamoja na dawa za kulevya.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano 16, 2024 na Kaimu Kamanda wa jeshi hilo mkoani Shinyanga, Kennedy Mgani, ambapo amesema operesheni hiyo imefanyika kuanzia Marchi 28 hadi Aprili 16 mwaka huu.

Amesema kwa kipindi hicho wamefanikiwa kukamata vitu mbalimbali vinavyodhaniwa kuwa ni vya wizi ambavyo ni mafuta ya dizeli lita 320, vipande 250 vya nondo, nyaya za umeme, matairi matano ya gari, injini moja ya pikipiki, pamoja na betri sita za magari.

Vitu vingine ni mashine moja ya kukata miti, pikipiki nne, mashine moja ya bonanza, redio mbili, mtungi wa gesi, na TV seti moja.

Aidha Kamanda Mgani amesema kuwa jeshi hilo pia limefanikiwa kukamata mitambo minne ya kutengeneza gongo, lita 13 za gongo, simu tano, vifaa vinavyosadikiwa kuwa ni vya kupigia ramli, pamoja na bangi kete 33.

“Baadhi ya watuhumiwa wa matukio haya tumewakamata na wengine tunaendelea kuwasaka, na upelelezi ukimalika watafikishwa mahakamani,” amesema Mgani.

Akizungumzia juu ya mafanikio ya kesi ambazo wamewahi kuzifikisha mahakamani, Kamanda Mgani amesema: “…kesi tulizofanikiwa mahakamani, ni pamoja na kufungwa kwa watu wawili baada ya kuwa tumewakamata na bangi.”

“Mmoja amefungwa miaka miwili na mwingine amefungwa miaka mitatu. Pia Kesi zingine ambazo wamefanikiwa, ni ya ubakaji; ambalo mhusika amefungwa miaka 30 jela” amesema na kuongeza;

“Pia kuna kesi zingine mbili, moja ikiwa ni ya kuvunja nyumba na kuiba, ambapo mshtakiwa amefungwa miaka miwili jela, huku kesi ya kuharibu mali mhusika amefungwa mwaka mmoja.”

Katika hatua nyingine amesema kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, jeshi hilo limefanikiwa kukamata jumla makosa 3,771 ya ukiukaji wa sheria za usalama barabarani ambapo wahusika waliwajibishwa na kulipa faini za papo kwa papo.

Ametoa wito pia kwa wananchi wa Shinyanga, kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, kwa kutoa taarifa mbalimbali za uharifu ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria na Mkoa uendelee kuwa Shwari.