Rais Guinea Bissau azuru nchini kwa siku tatu, kutembelea SGR

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:29 AM Jun 21 2024
RAIS wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embalo
Picha: Mtandao
RAIS wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embalo

RAIS wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embalo, anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini leo, huku akitarajia kutembelea mradi wa treni ya kisasa (SGR).

Kadhalika, nchi hiyo ambayo imefanikiwa katika biashara ya korosho kuuza nje ya nchi kwa asilimia 90, ujio wa rais huyo pia utatoa uzoefu wa namna walivyofanikiwa kwenye zao hilo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Samwel Shelukindo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salam jana, alisema ujio huo utaimarisha uhusiano na biashara.

“Urari wa kibiashara hauko vizuri sana, kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 urari wa biashara haukuzidi dola 200,000 hivyo mkakati utakaoanzishwa utakuza biashara, kwa wananchi wetu kupeleka kule bidhaa,” alisema Dk. Shelukindo.

Alisema baada ya kuwasili nchini atapokewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Waziri January Makamba, na baadaye Ikulu na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan.

“Ingawa kipaumbele pia ni katika kukuza biashara kwenye zao la korosho, wao wamefanikiwa katika zao hili, ili tujifunze, ushirikiano katika uzalishaji wa zao la korosho.”

Balozi Dk. Shelukindo aliongeza kwamba pia ajenda zingine ni pamoja na masuala yanayohusu udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA) na ushirikiano katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Alisema Rais EmbalĂł, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ALMA, atafafanua ziara kwenye ofisi za taasisi hiyo zilizopo nchini, ili kupanga mikakati ya kupanua wigo wa taasisi, ambayo ilianzishwa mwaka 2009 na viongozi wa nchi 55 za Afrika, kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo, ifikapo mwaka 2030. 

“Tanzania na Guinea Bissau, zimedhamiria kuimarisha na kuinua kiwango cha ufanyaji biashara na uwekezaji hususan kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), nchi zote mbili zimeridhia uanzishwaji wa eneo hilo. 

“Itakumbukwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwaka 2023, Mwenyeki, Rais EmbalĂł alizitambua nchi sana, ikiwamo Tanzania kwa kubuni matumizi bora ya Kadi ya Alama ya ALMA (ALMA Scorecard) inayosisitiza uwajibikaji. 

Akizungumzia kuhusu uzalishaji wa zao la korosho, alisema Guinea Bissau imejikita katika uzalishaji wa zao hilo ambalo nchi hiyo huuza zaidi nchini India.  

“Thamani ya uuzaji nje wa zao hilo inafikia takribani asilimia 90 pia zao hilo ni chanzo kikuu cha mapato kwa wakulima wadogo wa nchi hiyo, kwa asilimia 80 na huchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa la Guinea Bissau.

“Inatarajiwa kupitia ziara hii, suala la uzalishaji wa zao la korosho ambalo pia hulimwa hapa nchini, hususan katika mikoa ya Kusini ikiwamo Mtwara na Lindi, litajadiliwa kwa kina,” alisema Balozi huyo. 

Pia, alisema Rais EmbalĂł na ujumbe wake watatembelea Miundombinu ya Reli ya Kisasa katika Kituo cha Stesheni, jijini Dar es Salaam na Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA).