RC Macha: Wapotoshaji chanjo ya HPV kukiona

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:08 PM Apr 22 2024
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizindua Kampeni ya Utoaji Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya Kizazi HPV mkoani humo.
PICHA: MARCO MSDUHU
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizindua Kampeni ya Utoaji Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Shingo ya Kizazi HPV mkoani humo.

MKOA wa Shinyanga waanza rasmi utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi (HPV), kwa watoto wa kike, huku serikali ikionya kuwa yeyote atakayebainika kupotosha kuhusu chanjo hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umefanyika leo Aprili 22, 2024 katika Shule ya Msingi Ndala “A” iliyopo Manispaa ya Shinyanga, mkuu wa mkoa huo, Anamringi Macha, amesema kumekuwa na desturi ya watu kupotosha juu ya chanjo mbalimbali.

“Chanjo hii ya saratani ya mlango wa shingo ya kizazi ni salama kabisa na haina madhara yoyote, na ilianza kutolewa tangu mwaka 2014, na tangu kipindi hicho hakuna madhara yoyote ambayo yametokea, sasa kwa wale ambao wataanza upotoshaji Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria,” amesema na kuongeza;

“Mwananchi yoyote ambaye hana uelewa kuhusu chanjo hii, ni vyema akafika kwenye vituo vya huduma za afya au maeneo ambayo chanjo inatolewa (mashuleni), aulize na kuelimishwa kuliko kuanza kuandika kwenye mitandao ya kijamii na kufanya upotoshaji au kwenye vijiwe, tukikubaini tutakuchukulia hatua.”

Aidha mkuu wa mkoa huyo amesema Serikali haiwezi kuleta chanjo yenye madhara kwa wananchi wake, na kwamba HPV imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), na kuwataka wazazi wasiwe na wasiwasi dhidi ya chanjo hiyo.

Mkoa wa Shinyanga umejiwekea lengo la kuwafikia watoto wa kike 198, 865; wenye umri wa kuanzia miaka 9 – 14; lengo likiwa ni kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi.

Hivyo ametoa wito kwa wazazi kuwaruhusu watoto wao wachanjwe ili kuwakinga na ugonjw ahuo, huku akiwataka walimu pamoja na wataalamu wa afya, kuhakikisha utoaji chanjo hiyo, auharibu vipindi vya masomo.

Katika hatua nyingine, Macha ametoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kujenga utaratibu wa kupima afya mara kwa mara, ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, na siyo kusubiri magonjwa hayo kuwa sugu au kupelekwa hospitali wakiwa hoi.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Yudas Ndungulile, amesema tayari chanjo zote zipo kwenye vituo, na kwamba zitatolewa katika maeneo ya shule za msingi na sekondari, pamoja na kwenye vituo vya afya.

Shadrack Geofrey, ambaye ni mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, ameupongeza mkoa huo kwa kufanya maandalizi mazuri ya utoaji wa chanjo hiyo, na kwamba ametembelea halmashauri zote na kujiridhisha maandalizi kuwa mazuri.

Naye Rose Mathias, mmoja wa wazazi, ameishukuru Serikali kwa kutoa chanjo hiyo ili kuwalinda watoto wao, huku akiwataka wazazi wana walezi kuwaruhusu watoto wa kike waliokusudiwa, kupata chanjo hiyo, kwakuwa wanakabiliwa na magonjwa mengi.

Naye Mwanafunzi Amina Hassani ambaye amepatiwa chanjo hiyo ya HPV, amesema amefarijika kuchanjwa na kwamba anaamini itamlinda dhidi ya ugonjwa tajwa.