RC Mtanda azindua mradi wa maji wa milioni 215 Magu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:52 PM Jun 19 2024
 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda (Kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited Obinna Anyalebechi (Kulia) wakizindua mradi huo wa maji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda (Kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited Obinna Anyalebechi (Kulia) wakizindua mradi huo wa maji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amezindua mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 215 katika Kijiji cha Kabila wilayani Magu mkoani humo.

Akizindua mradi huo hivi karibuni, Mtanda alisema mradi huo ni muhimu kwa wakazi wa Kijiji cha Kabila, kwani unakwenda kuondoa changamoto ya maji ya muda mrefu kwa kwenda kuhudumia zaidi ya wakazi 12,000.

Mradi huo umefadhiliwa na Kampuni ya Bia Serengeti na shirika lisilo la kiserikali, African Community Advancement Initiative (AFRIcai).

‘‘Mashirika haya binafsi yamekuwa mstari wa mbele katika kukuza miradi ya maendeleo nchini ambayo inawezesha kuwepo kwa jamii iliyo na uzalishaji na afya bora" alisema Mtanda na kuongeza;

‘‘Ushirikiano kati ya SBL na AFRIcai unathibitisha dhamira ya sekta binafsi kwa uwajibikaji wa kijamii na maendeleo endelevu. Kwa kuwekeza katika miradi inayolenga mahitaji msingi ya jamii kama usambazaji wa maji, SBL na AFRIcai wanadhihirisha dhamira yao ya kuboresha ustawi wa jamii ya watanzania na kuchochea mafanikio ya muda mrefu." alisema

Alisema mradi huo unahusisha ufungaji wa pampu ya kuzamisha ndani ya kisima, ujenzi wa nyumba ya pampu, tangi la kuhifadhi maji, mtandao wa mabomba ya maji, na vituo vipya vya maji 13 vyenye uwezo wa kutoa mita za ujazo 87,000 za maji kwa mwaka.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi alisema kuwa mradi huo ambao unajulikana, Water for Life (Maji kwa ajili ya uhai) ni miongoni mwa mikakati ambayo kampuni hiyo ya bia inaendesha katika mikoa ya Iringa, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mwanza, Singida, Mara, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam, Pwani na Dodoma ikiwa imewanufaisha zaidi ya watu milioni mbili kwa maji safi na salama.

“Mwaka huu, SBL kwa kushirikiana na African Community Advancement Initiative (AFRIcai), tumekamilisha ujenzi wa mradi huu muhimu wa maji katika kata ya Kabila, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza. 

Kwa kutambua kwamba maji ni hitaji la msingi la maisha na moja ya rasilimali muhimu zaidi, SBL kupitia mpango wake wa kusaidia jamii, imekuwa ikitekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kutoa maji bure kwa watu wanaoishi katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji nchini. 

Kupitia sera ya Water for Life hadi sasa tumetekeleza miradi 26 ya maji katika maeneo yenye uhaba wa maji katika sehemu mbalimbali za nchi, ambapo zaidi ya watu milioni 2 wamenufaika na miradi hii ambayo inalenga kutoa maji safi na salama.” alisema 

Nae Meneja wa Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu alisema, “Mradi wa Kabila sio tu kwamba utaboresha afya za wakazi wa eneo hilo bali pia utaongeza tija kiuchumi hususani kwa watoto wa kike na wanawake ambao hawatahitaji kutumia saa nyingi kutafuta maji safi na salama sehemu nyingine. Hii inawapa fursa ya kuhudhuria shule  wakiwa huru.” alisema