RIPOTI MAALUM -3 Wafanyakazi wa kiwanda cha UFI wasotea stahiki zao kwa miaka 26

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:28 AM Jun 19 2024
Mwonekano wa majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Zana za Kilimo UFI (Ubungo Farm Implements), yaliyopo upande wa kushoto mwa Kituo cha Mwendokasi Shekilango, barabara ya Morogoro. Kwa sasa ni kiwanda cha mabomba cha TSP Limited (Tanzania Steel Pipe).
Picha: Maktaba
Mwonekano wa majengo ya kilichokuwa Kiwanda cha Zana za Kilimo UFI (Ubungo Farm Implements), yaliyopo upande wa kushoto mwa Kituo cha Mwendokasi Shekilango, barabara ya Morogoro. Kwa sasa ni kiwanda cha mabomba cha TSP Limited (Tanzania Steel Pipe).

HII ni sehemu ya tatu ya ripoti inayoangazia kiwanda cha UFI (Ubungo Farm Implements) kilichoko Shekilango, wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam, ambacho hivi sasa kinazalisha mabomba ya maji.

Hali hiyo inakinzana na dhamira ya mwasisi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye serikali yake ilikianzisha kwa lengo la kuzalisha zana za kilimo ili kuhakikisha wakulima wanakuwa na uhakika wa kuzipata kwa urahisi nchini na kwa bei nafuu. Endelea na sehemu ya mwisho ya ripoti hii... 

Kwa miaka 26 wafanyakazi wa kiwanda hicho wanasotea haki zao. Wanadai wameshaandika zaidi ya barua 40 kwa mamlaka mbalimbali nchini tangu mwaka 1998 bila mafanikio yoyote.

Hadi kiwanda kinabinafsishwa mwaka 1998, kilikuwa na wafanyakazi 508 wanaodai stahiki zao za malipo ya mishahara, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na posho nyinginezo.

Taasisi ambazo wamekuwa wakielekeza barua zao kushughulikia madai yao ni pamoja na Bunge na Ikulu. Hata hivyo wanadai hawajui tarehe ya kulipwa stahiki zao.

Katibu wa Kamati ya Ufuatiliaji Mafao ya Wafanyakazi wa Kiwanda cha UFI, Makamba Kigome, anasema wanachodai ni kupunjwa katika malipo ya mtumishi na familia zao - kwamba hayakulipwa kulingana na umbali wa kila mmoja anakotoka, pia kutozingatiwa ngazi ya mshahara wa mtumishi.

Madai mengine ni posho ya kufungasha mizigo; haikuwafikia watumishi licha ya kuwapo kwenye mchanganuo wa malipo ya UFI.

Kigome anataja hoja zingine ni kutofuatwa Mkataba wa Hali Bora Sehemu ya Kazi, malimbikizo kulipwa kwa kutofuata mabadiliko ya mishahara tangu Julai 1994 hadi Julai 1998, kutolipwa malimbikizo ya likizo badala yake walilipwa likizo moja pekee ya mwaka 1994.

Wafanyakazi hao pia wanadai posho ya kujikimu kwa kipindi cha miezi mitatu wakati wanasubiri kulipwa mafao ya kuachishwa kazi.

Mwandishi ameona nakala za barua 30 kati ya 41 ambazo wafanyakazi hao wanadai kuzielekeza kwa mamlaka mbalimbali za serikali kukumbushia madai yao.

Pamoja na taasisi zingine, barua hizo zimeelekewa kiwanda cha UFI wakati huo, Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) na uliokuwa uongozi wa UFI.

Mathalani, barua yenye kumbukumbu PSRC/1/13/143 ya Mei 2002 kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa PSRC kwenda kwa Kamishna wa Kazi Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, ina maudhui ya madai ya waliokuwa wafanyakazi wa UFI, Linus Kupuya na wenzake 507.

Katika barua hiyo mnaelekezwa kuwa madai ya wafanyakazi hao yako nje ya utaratibu uliowekwa kwa mashirika yaliyobinafsishwa na serikali, hivyo hayatekelezeki.

"Sera iliyopo ni kwamba serikali inapolazimika kulipa mafao ya wafanyakazi badala ya kampuni ambayo ndio mwajiri wao, inalipa mafao ya kisheria tu. 

"Ufafanuzi umekuwa ukitolewa mara nyingi kwa wahusika kupitia taasisi mbalimbali za serikali ikiwa ni pamoja na Waziri wa Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara," inasomeka barua hiyo ambayo mwandishi wa habari hii ameona nakala yake.

Katika barua hiyo, Mtendaji Mkuu wa PSRC anaeleza, "Malipo kwa mujibu wa stahili za kisheria ni mshahara wa mwezi mmoja ikiwa ni notisi ya kuachishwa kazi, malipo ya likizo isiyozidi ya kipindi cha mwaka mmoja, nauli ya likizo isiyozidi kipindi cha mwaka mmoja, nauli ya mfanyakazi na familia yake hadi sehemu alikozaliwa - ya mizigo na makazi.

"Pia gharama za kusafirisha mizigo kwa kiwango cha kanuni za uajiri, pamoja na malimbikizo ya mishahara ambayo mfanyakazi anakuwa ametumikia na hajalipwa."

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa PSRC, serikali iliwasilisha michango ya akiba ya wafanyakazi ambayo ilikuwa haijawasilishwa kwenye mamlaka zinazohusika na waajiri wao.

Anaeleza katika barua hiyo kuwa wafanyakazi hao wanadai marupurupu yanayotokana na mkataba wa hiari kati yao na uongozi wa UFI, kiinua mgongo, gharama za ufungaji mizigo, notisi za kuachishwa kazi za miezi miwili na malimbikizo ya likizo zinazozidi moja.

"Kama utakavyoona madai ya aina hii hayapo kwenye orodha ya yale yanayostahili kulipwa na serikali chini ya sheria inayoongoza urekebishaji mashirika ya umma kwa sababu marupurupu ya mkataba wa hiari yanatakiwa yatokane na juhudi za uzalishaji za wafanyakazi wenyewe.

"Makubaliano haya ni kugawana sehemu fulani ya ziada inayotokana na uzalishaji mzuri. Wafanyakazi hawa walishalipwa mafao yao ya pensheni na mfuko wa pensheni wa mashirika ya umma kama inavyotakiwa. 

"Mfanyakazi hawezi kuhusishwa na mpango zaidi ya mmoja wa pensheni au wa akiba ya uzeeni, na madai ya gharama za ufungaji mizigo na malimbikizo ya likizo zinazozidi moja hayapo katika utaratibu uliotajwa hapo juu," anaeleza Dk. H. Kavishe, Mtendaji Mkuu wa PSRC wakati huo, katika barua hiyo wakati akimjibu Kamishna wa Kazi wa wizara.

Katika barua yao ya Februari 14 mwaka huu waliyomwandikia Spika wa Bunge, Dk. Tulia Askon, waliokuwa wafanyakazi 271 wa kiwanda cha UFI, wanaeleza kuwa baada ya mchakato wa ubinafsishaji, walilipwa sehemu ya malimbikizo ya mishahara ya miezi sita kwa wafanyakazi 271 waliokuwa kazini na miezi 49 kwa wafanyakazi 237 waliokuwa likizo.

Katika barua ya Wizara ya Viwanda yenye kumbukumbu namba MIT-C/I.40/77 ya Agosti 16, 1998, Kaimu Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo, Kingunge Ngombale Mwiru (marehemu), alimwandikia barua Waziri wa Fedha wakati huo, Daniel Yona, akimweleza ulipaji wafanyakazi wa UFI utakavyofanyika.

Katika barua hiyo, Waziri Kingunge anasema, "Ninapenda nipendekeze kwako kwamba ulipaji mafao ya wafanyakazi ufanyike kwa awamu mbili; kwanza walipwe malimbikizo ya mishahara ili waweze kujikimu na baadaye walipwe mafao yao baada ya uchambuzi wa kina kufanywa na wataalamu."

Katika barua yao Februari 14 mwaka huu kwa Spika, waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho wanamweleza Spika kuwa:

"Malipo ya mafao hayakufanyika kabisa kwa wafanyakazi wote. Kwa wale wafanyakazi waliokuwa wametimiza masharti ya kuwa ‘pensionable’ (kulipwa mafao), yaani walikuwa wametumikia kiwanda zaidi ya miezi 120 (kwa vigezo vya Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF) na NPF) wakaingizwa katika mpango wa kulipwa pensheni kila mwezi 'kiainaaina', ambapo pia ukasitishwa na serikali kwa waliokuwa chini ya umri  wa miaka 55."

Wafanyakazi hao wanasema katika barua hiyo kuwa wanachodai ni haki zao za msingi walizodhulumiwa. 

Wanasema mafao wanayodai ni haki zao kwa kuwa walijiunga katika mifuko ya jamii ya PPF na NPF na wakachangia michango yao kutoka katika mishahara yao kwa mujibu wa sheria.

"Hatuombi kutoka nje ya hilo. Tunachohitaji ni mapunjo ya haki zetu pamoja na mafao yetu. Malipo hayo yalipwe kwa thamani ya Shilingi ya sasa," wafanyakazi hao wanadai.

Wanadai wamefikisha malalamiko yao sehemu zote husika, zikiwamo Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Ofisi ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, madai yao hayajafanyiwa kazi.

"Inatusikitisha na kutuumiza sana tunapoendelea kuzungushwa kupata stahiki zetu, hii imetufanya tuwe tegemezi na ombaomba katika jamii ambayo tuliitumikia kwa moyo na uadilifu mkubwa sana. 

"Baadhi ya wenzetu wameshatangulia mbele ya haki kwa kukosa uwezo wa kujihudumia kimaisha na kimaendeleo wao na familia zao.

"Hivi tumekosa nini hata tuadhibiwe na kunyanyaswa namna hii kwa miaka zaidi ya 26 sasa? UFI na Urafiki ni viwanda vya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipata msaada toka China, tunaomba tulipwe kama walivyolipwa wenzetu wa Urafiki.

"Tunaomba utusaidie mahesabu haya baada ya kujiridhisha Bunge letu tukufu limshauri Rais Samia Suluhu Hassan atulipe madai yetu ambayo ni ya muda mrefu tuweze kupata malipo yetu kwani imekuwa muda mrefu sasa tumekuwa tukipeleka malalamiko yetu sehemu mbalimbali serikalini bila kupatiwa haki zetu za msingi.

"Tunaendelea kuishi katika hali ngumu inayohatarisha maisha yetu na familia zetu kutokana na uamuzi wa watu wachache kwa utashi wao binafsi," wafanyakazi hao wanalalama.

Katika barua hiyo, wafanyakazi hao pia wanadai UFI haikuonesha mali ambazo ni majengo, madeni waliyokuwa wanadai kwa kuwa kiwanda hakikuruhusiwa kuuza moja kwa moja kwa wateja bali waliuza kwa mkopo, pia fedha zilizobaki kwenye akaunti za kiwanda na bidhaa ambazo zilikuwa hazijaisha.