Rufiji, Kibiti zatahadharishwa huku misaada ikizidi kutolewa

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 07:56 PM Apr 17 2024
Baadhi ya waathirika mafuriko wilayani Rufiji, pamoja na misaada iliyotolewa.
Picha: Julieth Mkireri
Baadhi ya waathirika mafuriko wilayani Rufiji, pamoja na misaada iliyotolewa.

Misaada ya kibinadamu imeendelea kutolewa kwaajili ya waathirika wa mafuriko yaliyozikumba wilaya za Rufiji na Kibiti, mkoani Pwani, huku Serikali ikiwataka wakazi wa wilaya hizo kuchukua tahadhari kwa kuondoka maeneo hatarishi, na hivyo kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na mvua kuendelea kunyesha.

Tahadhari hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Selemani Jafo, alipotembea Wilaya ya Rufiji yalipotokea mafuriko ambapo pia alishiriki kupokea msaada wa nishati safi pamoja na chakula kutoka kampuni ya Lake Agro.

Jafo amesema wananchi ambao bado wapo maeneo hatarishi wanatakiwa kuondoka kuepuka madhara ambayo yanaweza kuwapata katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha na kusababisha mafuriko.

Aidha waziri huyo ameipongeza kampuni ya Lake Agro kwa kutambua umuhimu wa nishati safi na kutoa mitungi 300 ya gas kwa ajili ya waathirika wa mafuriko sambamba na tani 20 za unga pamoja na mafuta ya diesel.

Akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameshukuru kampuni hiyo huku akiwaomba kupeleka maombi kwa kampuni rafiki ili nao waweze kusaidia waathirika hao ambao kwasasa wanaishi kwenye makambi.

Kunenge pia ametoa maelekezo kwa wananchi ambao wapo maeneo hatarishi wasisubiri kuokolewa badala yake waondoke katika maeneo hayo kabla madhara makubwa hayajawafikia.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amemshukuru kwa msaada huo huku akisema wananchi ambao wapo kwenye kambi walikuwa na changamoto ya kuandaa chakula na kwamba upatikanaji wa mitungi hiyo ya gesi, utawasaidia katika kipindi hiki cha mvua.

Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa makampuni ya Lake group, Meneja wa Lake Agro, Nasoro Abubakar, alisema msaada huo umetokana na kuguswa na mafuriko yaliyotokea na kusababisha madhara kwa wananchi.

Abubakar amesema wanatambua juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na uongozi wa Mkoa wa Pwani katika kupeleka misaada mbalimbali ya chakula tangu mafuriko hayo yalipotokea, jambo liliwafanya kuunga mkono.

Kampuni hiyo ambayo ni moja ya wawekezaji katika mkoa huo, imekabidhi unga sembe kilo 20,000 (tani 20), mafuta ya diesel lita 2500 na mitungi ya gesi mitungi 300 kwa waathirika wa mafuriko Rufiji.